Na Farida Mangube Morogoro
Wakazi wa Kitongoji cha Kichangani, Kijiji cha Mamboya katika Kata ya Gairo, Wilaya ya Gairo, wameondokana na changamoto ya muda mrefu ya mafuriko na kukatika kwa mawasiliano baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa daraja na mtaro wa maji wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 455.
Mradi huo uliotekelezwa na wakala ya Barabara za vijjini na mjini TARURA umezinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Kata hiyo waliokuwa wakikabiliwa na adha ya mafuriko yaliyokuwa yanakatiza mawasiliano na kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hususani wakati wa masika.
Akisoma taarifa ya Mradi kwa mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa Mhandisi Happnes Mbuge kutoka TARURA WIlaya ya Gairo amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa daraja moja, mtaro wa maji wenye urefu wa mita 330 pamoja na gabioni za kuimarisha kingo za mtaro.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kulidhishwa na mradi huo kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ndugu Wazo Michael Mwang’onda amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora inayowezesha maendeleo na kuboresha maisha yao.
“Mwenge wa Uhuru umejionea kazi kubwa iliyofanyika hapa Kichangani. Huu ni mradi wenye manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuwa umeondoa changamoto ya mafuriko na kukatika kwa mawasiliano iliyokuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo katika eneo hili. Tunawapongeza wote walioshiriki kufanikisha utekelezaji wake,” alisema Mwang’onda.
Ameongeza kuwa maendeleo ya kweli hujengwa kupitia miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Tunapozindua mradi kama huu tunatarajia kuona ongezeko la shughuli za kiuchumi, urahisi wa upatikanaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Jukumu la kuutunza sasa ni la wananchi wenyewe,” alisema.
Mhandisi Simon Masala ni Meneja wa TARURA Wilaya ya Gairo amesema Mradi huo unatarajiwa kuongeza usalama wa makazi ya wananchi, kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Kitongoji cha Kichangani, Kijiji cha Mamboya na Wilaya ya Gairo kwa ujumla.
Kwa upande wao, wananchi wa Kichangani wameeleza furaha yao baada ya kukamilika kwa mradi huo wakisema umemaliza tatizo ambalo kwa miaka mingi lilikuwa likiwasababishia hasara na usumbufu mkubwa.
Othuma Yusuf ni Mmoja wa wakazi wa Kata hiyo amesema kabla ya ujenzi wa daraja na mtaro huo, mafuriko yalikuwa yakikatiza mawasiliano kati ya Kichangani na maeneo mengine ya Wilaya ya Gairo, hali iliyokuwa ikiathiri biashara, elimu na huduma za afya.
“Tulikuwa tunapata shida kubwa sana wakati wa mvua. Maji yalifurika na kufanya usafiri kuwa mgumu au kukatika kabisa. Wakulima walishindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, wafanyabiashara walikosa wateja na hata wagonjwa walipata changamoto ya kufikishwa hospitali kwa wakati. Kwa kweli tulikuwa tunaumia sana,” alisema Othuma.
Naye Jane Joseph amesema changamoto hiyo ilikuwa ikisababisha wananchi wengi kupoteza fursa za kiuchumi kutokana na kushindwa kufikia masoko na maeneo ya biashara kwa wakati.
“Kipindi cha masika kilikuwa kigumu sana kwetu. Wakati mwingine mazao yaliharibika kwa kuchelewa kufikishwa sokoni na biashara nyingi zilisimama kwa sababu ya kukosekana kwa mawasiliano ya uhakika. Mradi huu umetufungua njia mpya ya maendeleo na tunaamini utaongeza kipato cha wananchi wengi,” alisema Jane.
Aliongeza kuwa pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi, daraja hilo litasaidia wanafunzi kufika shule kwa urahisi na wananchi kupata huduma za afya bila vikwazo vinavyotokana na mafuriko.
Wananchi hao walitoa shukrani kwa Serikali kwa kupeleka fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo, wakisema umekuwa mkombozi mkubwa kwa jamii ya Kichangani na maeneo jirani.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...