Na Janeth Raphael MichuziTv- Bungeni Dodoma

Serikali ya Tanzania imeeleza mkakati wake wa kuendeleza na kutenga Maeneo Maalum ya Uwekezaji (Special Economic Zones – SEZs) kwa lengo la kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kupitia uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na miundombinu wezeshi.

Hayo yameelezwa Bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt.Pius Chaya

alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Itigi, Yohana Stephen Msita, aliyehoji kuhusu hatua za Serikali katika kutenga ardhi na kulipa fidia kwa ajili ya maeneo hayo ya uwekezaji.

Dkt. Chaya amebainisha kuwa Serikali, kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), inaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kutambua, kutenga na kuendeleza maeneo ya kimkakati ya uwekezaji kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali.

Taasisi hizo ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha ardhi inapatikana kwa wakati, fidia inalipwa ipasavyo, na maeneo yanakuwa tayari kwa matumizi ya uwekezaji.

Mkakati huo unahusisha hatua muhimu zikiwemo utambuzi wa maeneo yenye fursa za kimkakati, uandaaji wa mipango kabambe ya matumizi ya ardhi, kufanya upembuzi yakinifu (feasibility studies), pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika uendelezaji wa maeneo hayo kwa kujenga miundombinu muhimu kama barabara, maji na umeme.

Kwa mujibu wa Serikali, hadi kufikia Mei 2026, jumla ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi 34 yamekwisha tangazwa katika maeneo mbalimbali nchini. Kati ya hayo, maeneo 16 yako chini ya usimamizi wa TISEZA, 12 yanamilikiwa na sekta binafsi, 4 yanasimamiwa na Halmashauri za Serikali za Mitaa (LGAs), na 2 yanamilikiwa na taasisi za umma.

Serikali pia imeeleza kuwa inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha maeneo hayo yanaendelezwa na kuvutia wawekezaji, ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na ajira nchini.

Aidha, imezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinayalinda maeneo yote yaliyotengwa kwa uwekezaji—ikiwemo yale yaliyolipiwa fidia na yale yanayosubiri malipo—ili kuzuia uvamizi na kupunguza migogoro ya ardhi.

Serikali imesisitiza kuwa ulinzi na usimamizi madhubuti wa maeneo hayo ni msingi muhimu wa mafanikio ya mkakati wa Maeneo Maalum ya Uwekezaji nchini.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...