Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mohamed Salum, amesema kuwa usafiri wa meli ya MV Liemba una umuhimu mkubwa kwa wananchi wanaotegemea huduma za usafiri wa majini katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, huku akieleza kuwa meli hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Salum alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa meli ya MV Liemba mjini Kigoma katika maadhimisho ya Siku ya Mabaharia yanayoendelea mkoani humo.
Amesema kuwa wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika wanategemea usafiri wa majini kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hivyo kukamilika kwa ujenzi wa meli hiyo kutasaidia kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji wa bidhaa.
“Meli ya MV Liemba ni muhimu kwa wananchi wetu kwa sababu inatoa huduma zinazogusa maisha ya kila siku ya watu wengi. Kukamilika kwake kutaimarisha usafiri salama na wa uhakika katika maeneo yanayohudumiwa na meli hiyo,” amesema Salum.
Aliongeza kuwa katika mkoa wa Kigoma, MV Liemba itaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuchochea shughuli za biashara, kuunganisha jamii na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wa ukanda huo.
Salum amesema uwekezaji unaofanyika katika kuboresha meli hiyo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya usafiri wa majini na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazochangia ukuaji wa uchumi wa bluu nchini.
Ziara hiyo ni sehemu ya shughuli za Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia ambayo yanalenga kutambua mchango wa mabaharia na wadau wa sekta ya usafiri wa majini katika maendeleo ya taifa.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...