Wataalamu wa afya, watafiti, viongozi wa vijana na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha huduma na sera za afya kwa vijana balehe barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mtandao wa ARISE kupitia Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Afya ya Umma, Dkt. Mary Mwanyika Sando, Juni 22, 2026, inaeleza kuwa Mkutano wa 2026 wa Afya ya Vijana Balehe Kusini mwa Jangwa la Sahara (CAH-SSA) pamoja na Mikutano ya Mwaka ya Mtandao wa Utafiti, Sayansi ya Utekelezaji na Elimu Afrika (ARISE), unafanyika kuanzia Juni 22 hadi 25, 2026 Jijini Dar es Salaam.Mkutano huo unafanyika chini ya kaulimbiu “Kuonesha Mafanikio ya Afua Endelevu za Afya ya Vijana Balehe Zinazoongozwa na Jamii”, ukiwa na lengo la kuonesha matokeo ya tafiti na kujadili mbinu bora za kuboresha afya ya vijana.
Mgeni rasmi katika mkutano huo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Tanzania, Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe, ambaye amezungumzia namna matokeo ya tafiti yanavyoweza kutumika kuboresha sera za afya, kuimarisha huduma kwa vijana na kuongeza ushiriki wa vijana katika ubunifu na utekelezaji wa afua zinazowahusu.
Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, washirika wa maendeleo, viongozi wa vijana, watafiti, taasisi za utafiti na sekta binafsi kwa lengo la kujenga ushirikiano wa kuongeza matokeo chanya katika afya ya vijana barani Afrika.
Katika mkutano huo, vijana pia wamepewa nafasi kupitia Wawakilishi wa Bodi ya Ushauri ya Vijana Balehe na Vijana kwa ujumla (AYAB), akiwemo Mtanzania Bi. Mariam Surve na Bi. Mariam Yusuff kutoka Nigeria, ambao wanawakilisha sauti na mahitaji ya vijana katika uundaji na utekelezaji wa programu za afya.
Miongoni mwa maeneo yatakayojadiliwa ni matokeo ya miradi ya DASH na ARISE-NUTRINT inayolenga kuboresha afya ya vijana katika maeneo ya lishe, mazoezi, afya ya uzazi na afya ya akili. Miradi hiyo imefadhiliwa na Serikali ya Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya.
Aidha, mkutano huo unalenga kuimarisha mipango ya Mtandao wa ARISE kwa kipindi cha mwaka 2026–2027 kwa kuweka mikakati itakayowezesha afua za afya kwa vijana kuwa endelevu kifedha na kutekelezwa kwa upana katika ngazi za jamii, kitaifa na kikanda.
Wakizungumza kuhusu umuhimu wa mkutano huo, viongozi wa ARISE wamesema jukwaa hilo ni muhimu katika kuunganisha tafiti, matokeo yake, sera na utekelezaji wa programu zinazolenga kuboresha maisha ya vijana barani Afrika.
Mtandao wa ARISE ni ushirikiano wa taasisi za Afrika na mabara mengine unaolenga kuimarisha uwezo wa utafiti wa afya ya umma na kuendeleza utekelezaji wa afua zenye msingi wa ushahidi, ukiwa na zaidi ya taasisi 22 kutoka nchi mbalimbali Kusini mwa Jangwa la Sahara.



.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...