Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kufanya Mkutano wake Na. 4 wa mwaka wa fedha 2025/2026 kuanzia tarehe 15 Juni hadi 3 Julai 2026 jijini Mwanza, ambapo itajadili na kutoa maamuzi kuhusu rufaa na malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa na watumishi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma tarehe 10 Juni 2026, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John C. Mbisso, amesema kuwa kupitia mkutano huo, Tume itatoa fursa kwa warufani na warufaniwa walioomba kufika mbele ya Tume ili kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zilizowasilishwa katika rufaa zao.
Bw. Mbisso amesema hatua hiyo inatekelezwa kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, aidha Tume itapitia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu yake katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Pamoja na shughuli za mkutano, amesema Tume itafanya ziara katika baadhi ya taasisi za serikali zilizopo jijini Mwanza kwa lengo la kutoa elimu kwa waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika usimamizi wa rasilimali watu.
Vilevile ameeleza kuwa Tume itatoa elimu kwa watumishi wa umma katika taasisi hizo kuhusu haki na wajibu wao katika utekelezaji wa majukumu ya utumishi wa umma Sambamba na hilo, itapokea na kushughulikia malalamiko ya watumishi wa umma ambao hawakuridhika na maamuzi yaliyotolewa na waajiri, mamlaka za ajira au mamlaka za nidhamu.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)(d) kikisomwa pamoja na Kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, Marejeo ya Mwaka 2023, Tume ya Utumishi wa Umma imepewa mamlaka ya kupokea na kushughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma wasiokubaliana na maamuzi yaliyotolewa na waajiri, mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu katika utumishi wa umma.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...