Na Oscar Assenga, Tanga


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma (MB), amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha nchini kuendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii kwa kuanzisha na kuunga mkono mipango inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Akizungumza jijini Tanga wakati wa uzinduzi rasmi wa ushirikiano kati ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kupitia mpango wa “Cash Waqf”, Mwinjuma alisema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha za kufadhili elimu ya juu nchini.



Uzinduzi huo pia uliambatana na ufunguzi rasmi wa tawi la PBZ IKHLAS, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi.

“Ni muhimu taasisi za fedha nchini kuendelea kushiriki katika maendeleo ya jamii kwa kuunga mkono mipango itakayowanufaisha wananchi katika maeneo mbalimbali,” alisema Mwinjuma.



Aidha, aliipongeza PBZ kwa juhudi zake za kupanua huduma za kifedha katika maeneo tofauti nchini, akibainisha kuwa hatua hiyo inachangia kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi wa taifa.

Pia aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo huduma za akaunti, uwekezaji na mikopo, ili kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuboresha ustawi wa maisha yao.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, CPA Fahad Hamid, alisema benki hiyo iliyoanzishwa Juni 30, 1966, inakaribia kutimiza miaka 60 ya kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Alisema PBZ inaendelea kupanua wigo wa huduma zake nchini, ambapo kwa sasa imefanikiwa kufika katika mikoa minane ya Tanzania Bara, hatua inayolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi.



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alisema ushirikiano huo una lengo la kupanua vyanzo vya rasilimali fedha ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata ufadhili wa masomo, hususan wanaojiunga na mafunzo ya amali kupitia vyuo vya kati.



Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, makubaliano hayo yataongeza uwezo wa HESLB kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kusaidia kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi unaohitajika katika viwanda na sekta nyingine za uzalishaji.



Akifafanua kuhusu mpango wa “Cash Waqf”, Meneja wa Uzingatiaji wa Shariah wa PBZ IKHLAS, Dkt. Issa Mohamed, alisema mpango huo unatoa fursa kwa watu binafsi, taasisi, wahisani na wawekezaji kuchangia au kuwekeza fedha zitakazosaidia kuongeza upatikanaji wa ufadhili wa elimu ya juu kwa vijana wa Kitanzania.



Alisema kupitia ushirikiano huo, PBZ na HESLB wanatarajia kuweka mfumo endelevu wa ukusanyaji na uwekezaji wa fedha kupitia mpango wa “Cash Waqf”, hatua itakayoongeza upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu na kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kutimiza ndoto zao za elimu.

Ushirikiano huo unatajwa kuwa miongoni mwa mikakati muhimu ya kuongeza fursa za elimu kwa vijana na kuchangia maendeleo ya rasilimali watu nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...