Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka taasisi za kifedha nchini kubadili mtazamo katika utoaji wa mikopo kwa kuweka mkazo zaidi kwenye uaminifu, historia ya biashara na mwenendo wa miamala ya waombaji, badala ya kutegemea dhamana za mali zinazoonekana pekee.
Akizungumza leo Juni 12, 2026 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam, Rais Samia alisema wanawake na vijana wengi wamekuwa wakikosa fursa za kifedha licha ya kuwa na biashara zenye mafanikio na uwezo wa kurejesha mikopo.
Ameeleza kuwa sehemu kubwa ya wanawake na vijana hawamiliki mali kama nyumba, viwanja au magari vinavyoweza kutumika kama dhamana, jambo ambalo limeendelea kuwa kikwazo katika kupata huduma za mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha.
Rais Samia amesema makundi hayo yana rekodi nzuri za biashara, mauzo yanayoonekana na historia ya miamala inayothibitisha uwezo wao wa kuendesha shughuli za kiuchumi kwa mafanikio, hivyo yanastahili kupewa nafasi zaidi ya kupata mitaji.
Amezitaka benki na taasisi nyingine za kifedha kubuni mifumo ya kisasa itakayowezesha kutathmini uwezo wa wakopaji kwa kutumia taarifa za biashara na mwenendo wao wa kifedha ili kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika uchumi.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa uaminifu wa mteja ni rasilimali muhimu inayopaswa kupewa uzito mkubwa katika maamuzi ya utoaji wa mikopo, akionya dhidi ya kuwanyima wananchi fursa kwa sababu ya kutokuwa na mali zinazokubalika kama dhamana za kawaida.
Katika hatua nyingine, amezitaka taasisi za kifedha kuongeza uwazi kwa kuwapatia wananchi taarifa sahihi na za kueleweka kuhusu masharti ya mikopo kabla ya kuingia kwenye mikataba ya ukopaji.
Amesema ni muhimu kwa wakopaji kuelewa kiwango halisi cha mkopo, muda wa marejesho, viwango vya riba na gharama nyingine zote zinazohusiana na mkopo huo ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Rais Samia pia ameeleza kuwa mafanikio ya sekta ya fedha hayapaswi kupimwa kwa idadi ya watu waliounganishwa kwenye huduma za kifedha pekee, bali kwa kiwango ambacho huduma hizo zinachochea ukuaji wa biashara, kuongeza mitaji na kuboresha maisha ya wananchi.
Kauli hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi na kuweka mazingira bora yatakayowezesha sekta binafsi kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo ya taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua mabanda ya maonesho katika Maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...