Na Janeth Raphael MichuziTv

RAIS wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, ametembelea Kituo cha Kumbukumbu cha Wapigania Uhuru wa Afrika pamoja na Makaburi ya Mashujaa wa Namibia yaliyopo wilayani Kongwa mkoani Dodoma, katika ziara maalum ya kuenzi mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika.

Katika ziara hiyo yenye umuhimu mkubwa wa kihistoria, Rais Nandi-Ndaitwah ameongozana na ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Namibia, ukiwemo mawaziri, wabunge na maafisa mbalimbali wa serikali. Upande wa Tanzania, viongozi kadhaa wa Serikali walishiriki katika mapokezi hayo, akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, pamoja na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda.

Akiwa katika eneo hilo la kihistoria, Rais wa Namibia aliongoza shughuli ya uwekaji mashada ya maua katika makaburi ya wapigania uhuru wa Namibia waliopoteza maisha wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni, kama ishara ya heshima na kumbukumbu kwa mchango wao katika kuipigania nchi yao.

Akizungumza baada ya shughuli hiyo, Rais Nandi-Ndaitwah alisema Kongwa ina nafasi ya pekee katika historia ya Namibia kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi, akisisitiza kuwa taifa lake litaendelea kuthamini na kukumbuka msaada mkubwa uliotolewa na Tanzania katika kipindi hicho muhimu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Tanzania na Namibia kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja za maendeleo na uchumi, akieleza kuwa baada ya ushindi wa kisiasa, mataifa ya Afrika yanapaswa kuelekeza nguvu katika kupigania uhuru wa kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.

Rais huyo pia alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Namibia umejengwa juu ya misingi imara ya historia, mshikamano na damu ya mashujaa waliopigania uhuru, akibainisha kuwa urithi huo utaendelea kuwa daraja muhimu linalounganisha mataifa hayo mawili kwa vizazi vijavyo.

Ziara ya Rais Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania inatazamwa kama hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, huku ikitarajiwa kufungua fursa zaidi katika sekta za biashara, uwekezaji, utamaduni na diplomasia kwa manufaa ya pande zote.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...