Na Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuwatambua na kuwawezesha vijana nchini kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu na kuongeza fursa za kiuchumi na kijamii kwa kundi hilo muhimu la maendeleo ya taifa.
Akijibu swali bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Latifa Khamis Juwakali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema Serikali inalitambua kundi la vijana kama nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi.
Waziri Nanauka amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha vijana wanatambuliwa rasmi kupitia zoezi la Utambuzi wa Vijana (Youth Mapping) linaloratibiwa na Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana.
Ameeleza kuwa zoezi hilo litasaidia kupata takwimu sahihi kuhusu idadi ya vijana, mahitaji yao halisi, pamoja na changamoto zinazowakabili, hatua itakayosaidia kupanga na kutekeleza afua zenye tija zaidi katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji vijana kupitia wizara za kisekta, mashirika ya umma, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha vijana wanapata fursa za kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali imeweka mifumo ya upatikanaji wa mitaji yenye masharti nafuu, ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana pamoja na mikopo inayotokana na asilimia 4 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, ambayo hutengwa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kuimarisha programu hizo ili kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya taifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...