Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizofanikiwa kusambaza huduma ya umeme  vijijini, hatua ambayo imewezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo kutoka ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji, huku sasa juhudi zikielekezwa katika kufikisha umeme kwenye vitongoji.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Hogoro wilayani Kongwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Senyamule alisema serikali inatarajia kupeleka umeme katika vitongoji sita vya kata hiyo katika mwaka ujao wa fedha.

Alieleza kuwa matarajio ya serikali ni kuhakikisha vitongoji vyote vinapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030, jambo litakalosaidia kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

“Zamani wananchi walitegemea chemli na vibatari kwa ajili ya mwanga, lakini sasa serikali imeona umuhimu wa kupeleka umeme karibu na wananchi ili waweze kupata mwanga wa uhakika na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowaongezea kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.”

Katika sekta ya elimu, Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali ya Awamu ya Sita imefanikisha ujenzi wa shule nyingi zaidi kuliko vipindi vilivyotangulia, huku akiwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote wanapata fursa ya elimu.

Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuona kila Mtanzania anajua kusoma na kuandika katika miaka ijayo ili kuwaandaa wananchi kukabiliana na ushindani wa dunia ya sasa inayokua kwa kasi katika nyanja za sayansi na teknolojia.

“Dunia ya leo imekuwa kama kijiji kutokana na maendeleo ya teknolojia. Elimu na ujuzi ni nyenzo muhimu zinazoweza kumpa mtu fursa ya kufanya kazi na kuishi popote duniani”.

Aidha, Senyamule alisema serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha zahanati, vituo vya afya na hospitali pamoja na kuweka mazingira rafiki ya utoaji huduma.

Kutokana na maboresho hayo, alisema hakuna sababu ya wanawake wajawazito kujifungulia nyumbani kwani huduma bora za afya sasa zinapatikana karibu na wananchi, hatua inayolenga kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...