Na Janeth Raphael - MichuziTv

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) wameeleza jinsi mpango huo ulivyobadilisha maisha yao kwa kuwainua kiuchumi, kuwawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo, kusomesha watoto na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa kikundi cha Tuwe na Imani cha Kianga, Zanzibar, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Fatuma Ally Mohamed, akiwa katika Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma Jijini Dodoma amesema kabla ya kujiunga na TASAF baadhi ya kaya zilikuwa zikiishi katika mazingira magumu ya umaskini, hali iliyosababisha changamoto hata ya kupata mlo mmoja kwa siku.

Amesema kupitia ruzuku pamoja na mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na TASAF, wanufaika wengi wamefanikiwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowaongezea kipato na kuboresha ustawi wa familia zao.

“Leo hii kaya nyingi zimebadilika. Watu wameanzisha biashara, wanapata kipato na wanaweza kugharamia mahitaji muhimu ya familia zao ikiwemo elimu ya watoto,” alisema Fatuma.

Mbali na kuimarisha uchumi wa kaya, alisema wanufaika pia wamekuwa wakishiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii, ikiwemo ujenzi wa mitaro ya maji na miundombinu mingine, huku wakinufaika na kipato kinachotokana na kazi hizo.

Ameongeza kuwa mafanikio ya mpango huo yamechangia kuongezeka kwa mahudhurio ya watoto shuleni, baada ya familia nyingi kupata uwezo wa kugharamia mahitaji ya elimu yaliyokuwa kikwazo hapo awali.

Kwa upande wake, mnufaika wa TASAF kutoka Temeke, Zuena Khamis, aliwataka wanufaika kutumia ruzuku wanazopewa kwa malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza umuhimu wa kuelekeza fedha hizo katika shughuli za maendeleo na uzalishaji mali.

Amesema matumizi yasiyo na tija, ikiwemo kununua mavazi ya sherehe na vitu vya anasa, yanaweza kudhoofisha juhudi za kujikwamua kiuchumi na kupunguza manufaa ya muda mrefu ya mpango huo.

“Ruzuku hizi ni mtaji wa maisha bora. Zinapaswa kutumika kuanzisha biashara na shughuli za kuongeza kipato badala ya matumizi ambayo hayaleti maendeleo ya kudumu kwa familia,” amesema Zuena.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, alisema ameridhishwa na maendeleo makubwa yaliyofikiwa na wanufaika wa mpango huo katika maeneo mbalimbali nchini.

Amewahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali na kutumia fursa zinazotolewa na TASAF ili kukuza biashara zao na kujenga uchumi imara unaowawezesha kuondokana na umaskini kwa njia endelevu.

Mziray amesema mafanikio yanayoonekana kwa wanufaika wengi ni ushahidi wa namna TASAF inavyoendelea kuwa chombo muhimu cha kuimarisha maisha ya wananchi wenye kipato cha chini na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...