-TASAC, ZMA Zaongeza Juhudi Kutatua Changamoto za Mabaharia

Na Mwandishi Wetu ,Kigoma

Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua za kisera na kiutendaji ili kuboresha ustawi wa mabaharia nchini, ikiwemo kulinda haki zao za ajira, kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha wanapata stahiki zao kwa wakati, kutokana na mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa bluu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi Ali Said Bakar, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma.

Mhandisi Bakar alisema mabaharia ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta ya usafirishaji wa majini na uchumi wa taifa kwa ujumla, hivyo ni lazima changamoto zinazowakabili zipatiwe ufumbuzi wa haraka na wa kudumu.

Alisema Serikali inatambua kuwa baadhi ya mabaharia wamekuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo kunyanyaswa kazini, mishahara kutolipwa kwa wakati, ujira mdogo na ukosefu wa huduma muhimu kama bima na matibabu, hali inayohitaji usimamizi madhubuti kutoka kwa mamlaka husika.

“Maadhimisho haya yanatoa fursa ya kutafakari mchango wa mabaharia katika maendeleo ya nchi na kuonyesha dhamira ya Serikali ya kushughulikia changamoto zao kupitia sera, sheria na hatua za vitendo,” alisema.

Aidha, alizitaka taasisi zinazosimamia sekta ya usafirishaji wa majini kuhakikisha zinakuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki za mabaharia, ikiwemo upatikanaji wa bima, huduma za afya na mazingira salama ya kazi.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, alisema kufanyika kwa maadhimisho hayo mkoani humo ni ishara ya kutambua mchango wa Kigoma katika usafirishaji wa majini na maendeleo ya uchumi wa bluu.

Alisema maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miundombinu ya usafiri wa majini yameongeza kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mizigo kupitia njia za maji.

“Maadhimisho ya Mabaharia kwa Kigoma yameaksi sekta ya usafirishaji ya zaidi ya asilimia 70 ya mizigo kusafirishwa kwa kutumia njia za maji katika Mkoa wa Kigoma  jambo ambalo limeongeza umuhimu wa mabaharia katika uchumi wa taifa,” alisema Rugwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (ZMA), Fatma Said Sandali, alisema ZMA kwa kushirikiana na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kuendelea kuweka mifumo bora ya uratibu na usimamizi ili kutatua changamoto zinazowakabili mabaharia.

Alisema maadhimisho hayo pia ni sehemu ya kuenzi mchango wa mabaharia waliopoteza maisha wakiwa kazini na kuonyesha mshikamano kwa familia zao.

Sandali alibainisha kuwa katika kipindi cha maadhimisho hayo, wananchi watapatiwa elimu kuhusu taaluma ya ubaharia, fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji wa baharini na maziwa, pamoja na umuhimu wa kuzingatia misingi ya kazi yenye utu, weledi na usalama.

Aliwataka mabaharia kuendelea kuzingatia nidhamu, uzalendo na taaluma katika kutekeleza majukumu yao, akieleza kuwa dunia ya sasa inahitaji mabaharia wenye ujuzi wa hali ya juu na weledi wa kimataifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, alisema mabaharia ni nguzo muhimu ya sekta ya usafirishaji duniani na wanastahili kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo.

Alisema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafirishaji wa majini, ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Kisasa ya Kalema mkoani Katavi, ambayo inatarajiwa kuongeza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa bluu nchini.

Mandia alisisitiza kuwa pamoja na kutambua mchango wa mabaharia, ni muhimu kwao kuendelea kufuata sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kuongeza tija, usalama na ushindani wa sekta hiyo.

Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani mwaka huu yanatarajiwa kuhusisha utoaji wa elimu katika mialo ya uvuvi, shule na maeneo mbalimbali ya jamii kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu mchango wa mabaharia katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi na Uchukuzi  Zanzibar Mhandisi Ali Said Bakar akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC Nah.Mussa Mandia mara baada ya  kufungua  Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani mkoani  Kigoma .
Katibu Mkuu wa Wizara Ujenzi na Uchukuzi  Zanzibar Mhandisi Ali Said Bakar akizungumza katika Ufunguzi wa  maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani mkoani  Kigoma .




Matukio mbalimbali katika picha wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya 16 ya Siku Mabaharia Duniani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...