Na Janeth Raphael MichuziTv 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, ametoa maagizo ya kuchukuliwa hatua kwa maafisa rasilimali watu watakaobainika kusababisha ucheleweshaji wa upandishaji madaraja kwa watumishi wa umma, licha ya wahusika hao kutimiza vigezo vyote vinavyohitajika.

Prof. Shemdoe ametoa kauli hiyo leo wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka.

Amesema kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya maafisa rasilimali watu kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hali inayosababisha watumishi stahiki kukosa au kucheleweshwa kupanda madaraja kupitia mifumo ya kiutumishi.

“Watumishi wanaostahili kupandishwa vyeo hawapaswi kukosa haki zao kutokana na uzembe wa kiutendaji wa mtu mmoja,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Prof. Shemdoe ameeleza kuwa hata yeye binafsi aliwahi kukumbana na changamoto ya kucheleweshwa kupandishwa cheo kwa takribani mwaka mmoja kutokana na kutokukamilika kwa taratibu za kiutumishi kwa wakati.

Aidha, ameelekeza kufanyika kwa tathmini maalum kwa maafisa rasilimali watu wakuu wote waliohusika na ucheleweshaji wa upandishaji madaraja katika mwaka wa fedha 2025/2026, ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waliobainika na uzembe.

Prof. Shemdoe pia amewataka waajiri kuhakikisha wanatenga bajeti ya kushiriki Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, huku akisisitiza umuhimu wa maonesho hayo katika kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Bw. Juma Mkomi, amesema maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Umoja wa Afrika linalolenga kuenzi Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika.

Ameongeza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa, kuhamasisha ubunifu katika utoaji huduma, pamoja na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...