Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) zimesaini makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa Digital Transformation Centre (DTC) Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kukuza usawa wa kijinsia na maendeleo jumuishi nchini.

Makubaliano hayo yanaendeleza ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani kupitia GIZ, kwa lengo la kutumia teknolojia za kisasa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi huku yakihakikisha wanawake na wasichana wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Mradi wa DTC Tanzania unaendana na vipaumbele vya maendeleo vya taifa, ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023, Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Tanzania wa mwaka 2024–2034.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkazi wa GIZ nchini Tanzania, Anne Hahn, alisema kuwa teknolojia za kidijitali zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha wanawake kupata ujuzi wa kiufundi na ujasiriamali unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Hahn alisema kuwa wanawake wanapopata fursa ya kutumia teknolojia za kidijitali, huongeza uwezo wao wa kubuni suluhisho mbalimbali, kuanzisha biashara, kuzalisha ajira na kuchangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa. Alibainisha kuwa uwekezaji katika teknolojia unafungua milango mipya ya fursa kwa wanawake na wasichana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

“Wanawake wanapowezeshwa kutumia teknolojia za kidijitali, wanakuwa wabunifu, wajasiriamali na washiriki muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi,” alisema Hahn, akisisitiza kuwa ushiriki wao katika sekta ya teknolojia ni muhimu kwa maendeleo endelevu na jumuishi.

Aidha, ametoa wito wa kuendelea kuwekeza katika mafunzo ya ujuzi wa kidijitali na programu za ujasiriamali kwa wanawake na wasichana ili kuhakikisha wanapata fursa zinazotokana na mageuzi ya teknolojia duniani, huku akieleza kuwa uwezeshaji wa wanawake kupitia teknolojia si suala la usawa wa kijinsia pekee bali ni msingi muhimu wa kukuza ubunifu, ajira na ukuaji wa uchumi wa taifa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...