Na Janeth Raphael - MichuziTv -Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea msaada wa Euro milioni 20, sawa na Shilingi bilioni 60.7, kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo mkoani Songwe. Msaada huo ulirasimishwa kupitia utiaji saini wa mkataba kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, alisema mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama pamoja na huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo husika.
Alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, kuunganisha wateja wapya, kujenga mtambo wa kutibu majitaka, kununua magari ya kuvuta majitaka na kujenga miundombinu ya usafi katika taasisi za umma ikiwemo vyoo vya shule zilizochaguliwa.
Dkt. Mwamba ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika sekta za maji, afya, uhifadhi wa maliasili na mazingira, usimamizi wa fedha za umma pamoja na usawa wa kijinsia. Alisema misaada hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Aidha, amekumbusha kuwa wakati wa majadiliano ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Ujerumani yaliyofanyika Machi 20, 2024 jijini Dar es Salaam, Serikali ya Ujerumani iliahidi kutoa Euro milioni 70 kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali nchini.
Alieleza kuwa msaada uliosainiwa sasa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi hiyo na unaonesha kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.
Dkt. Mwamba amesisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza ushirikiano wa maendeleo na Ujerumani, huku akiahidi kuwa serikali itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha miradi yote inayofadhiliwa inatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi.
Naye Mkurugenzi Mkazi benki ya Maendeleo Ujerumani Vanessa Eidt amesema ushirikiano Baina ya Tanzania na Ujerumani utaendelea kuleta matunda kwa wananchi wa Tanzania na anaamini mradi huo utakqenda kutekelezwa kama ulivyopamgwa na kunufaisha wananchi wa maeneo hayo Kupata majie safi na ya uhakika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maji. mhandisi Mwajuma Waziri amesema mradi huo umefika wajati muafaka kwani kuna mabadiliko ya tabia nchi pamoja na ukuaji wa kasi wa miji inayoongwza shinikizo katika rasilimali za maji, hivyo utekelezaji wa mradi huo utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maji unaozingatia mabadikiko ya tabia nchi na kuboresha upatikanaji wa maji kwa uhakika katika maeneo hayo.
Hata hivyo Mhandisi Mwajuma amesema wizara ya maji itaendelea kuhakikisha mradi huo unatekelezaa kwa ufanisi, uwazie na kwa wakati kwa kushirikisha kwa karibu na wadau ili kuhakikisha unaleta manufaa ya kudumu kwa wananchi wa Tanzania.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...