Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuwa chachu ya mabadiliko kwa kaya maskini, hususan wanawake, kwa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuanza maisha ya kujitegemea.

Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani wa TASAF, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Uswege Edward, amesema taasisi hiyo imewashirikisha baadhi ya wanufaika wa mpango katika banda la maonesho ili kuonesha mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa TASAF Awamu ya Pili.

Amesema wanufaika hao kutoka Tanzania Bara na Visiwani wameweza kunufaika kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupata mitaji, vifaa vya uzalishaji na fursa zilizowasaidia kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazowaingizia kipato.

"Tunajivunia mafanikio ya walengwa wetu maana wakati wa usajili baadhi yao walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa za maisha, ikiwemo kushindwa kumudu milo mitatu kwa siku. Leo hii wengi wao wanaendesha biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazowapa kipato na kuwafanya wajitegemee", amesema Uswege.

Aidha, amesema TASAF inaamini imefanikiwa kuwasaidia walengwa wengi kuondokana na utegemezi na kuanza safari ya kujitegemea kiuchumi.

Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Devota Karia, ameishukuru TASAF kwa kuwapatia nafasi ya kushiriki katika maadhimisho hayo, akieleza kuwa yamekuwa fursa muhimu ya kutangaza biashara zao na kupata wateja wapya.

Pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuunga mkono na kuimarisha utekelezaji wa mpango wa TASAF, ambao umeleta matumaini mapya kwa maelfu ya kaya nchini.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...