Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imesema ipo katika hatua za Kuzindua kiwanda cha kisasa cha kuchakata mbolea Mkoani Tanga kitakachozalisha mbolea kulingana na kiwango cha rutuba ya udongo wa maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima na uzalishaji wa mazao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma Juni 23, 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TFC, Nuru Mhando, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kujengwa mkoani Tanga na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea zinazokidhi mahitaji halisi ya udongo wa kila eneo.

Amesema kupitia teknolojia ya upimaji wa udongo, kiwango cha rutuba kitafahamika kabla ya kutengenezwa mbolea maalum inayofaa kwa eneo husika, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa ufanisi zaidi.

“Kiwanda hiki kitazalisha mbolea kulingana na mahitaji ya udongo wa maeneo tofauti nchini, hii itasaidia wakulima kupata mbolea sahihi na kuongeza mavuno kwa gharama nafuu.”

Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa kiwanda hicho kutapunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama za uagizaji, huku kikichangia upatikanaji wa mbolea bora kwa wakati unaohitajika.

Mhando amesema TFC ni kampuni ya serikali inayosambaza mbolea kwa wakulima kupitia mfumo wa ruzuku, ambapo serikali huchangia sehemu ya gharama za mbolea ili kuwasaidia wakulima kuzipata kwa bei nafuu.

Amesema kampuni hiyo imeendelea kusambaza mbolea za mazao ya chakula na nafaka, ambapo hadi sasa zaidi ya tani 49,000 za mbolea za kupandia na kukuzia mazao zimesambazwa kwa wakulima nchini, pia imekuwa ikitoa mbolea kwa wakulima wa tumbaku, moja ya mazao ya kimkakati nchini.

Aidha, amesema TFC inaendelea kutoa mafunzo kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kuhakikisha pembejeo hizo zinatumika kwa manufaa makubwa.

Amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, hatua itakayochangia upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuimarisha uchumi wa wananchi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...