Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema matumizi ya gesi asilia nchini yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, hali inayochochea maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi pamoja na kuongeza manufaa kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 23, 2026, katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Eng. Charles Sangweni, amesema ongezeko hilo limechangiwa na juhudi za Serikali zinazoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Eng. Sangweni amesema mwenendo wa matumizi ya nishati duniani unaonesha kuwa katika miaka ijayo matumizi ya mafuta ya petroli na dizeli yanaweza kupungua kutokana na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la matumizi ya magari ya umeme pamoja na yale yanayotumia gesi asilia.

Amesema hali hiyo inaifanya gesi asilia kuwa rasilimali muhimu zaidi katika kipindi hiki cha mpito huku Tanzania ikiwa na fursa kubwa ya kunufaika kutokana na akiba yake ya gesi na mahitaji yanayoendelea kuongezeka katika soko la ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa pamoja na mabadiliko ya teknolojia duniani yanayochochea matumizi ya magari ya umeme na yale yanayotumia gesi asilia, Tanzania bado ina nafasi kubwa ya kunufaika na rasilimali zake kutokana na mahitaji yanayoendelea kuongezeka.

Sangweni amesema PURA imeendelea kupata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake kwa kusimamia utekelezaji wa mikataba ya utafutaji, uchimbaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, hatua ambayo imechangia kuongeza mapato ya serikali kupitia mirabaha, kodi na vyanzo vingine vya mapato.

Aidha, amesema wananchi wanaendelea kunufaika kupitia utekelezaji wa sera za maudhui ya ndani (Local Content), ambapo Watanzania wanapewa kipaumbele katika zabuni za huduma, bidhaa na ajira zinazotokana na shughuli za sekta ya mafuta na gesi.

Amesisitiza kuwa PURA itaendelea kusimamia kwa karibu shughuli zote za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya taifa na kuchangia mapato.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...