Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Dodoma imeendesha zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Miyuji B, iliyopo eneo la Mpamaa jijini Dodoma Juni 28,   2026, ikiwa ni sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TRA pamoja na Tuzo za Rais kwa Walipakodi Bora. Zoezi hilo linalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Pendolake Elinisafi, amesema katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa TRA, Mamlaka imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma kwa walipakodi kupitia maboresho ya mifumo ya kidijitali, ikiwemo Mfumo wa IDRAS, ambao umerahisisha ulipaji wa kodi, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Elinisafi amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya mifumo ya utoaji huduma, matumizi ya teknolojia pamoja na kujituma kwa watumishi wa TRA katika kuwahudumia walipakodi kwa weledi na ufanisi.

Aidha, amewapongeza watumishi wa TRA kwa mchango wao mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, akieleza kuwa fedha zinazokusanywa kupitia kodi zimeendelea kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwemo uboreshaji wa huduma za elimu, afya, ujenzi wa barabara na miundombinu mingine muhimu inayowanufaisha wananchi.

Amesema maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanatoa fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 1996, huku yakichochea dhamira ya kuendelea kuboresha huduma kwa walipakodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa maendeleo ya Taifa.

Akizungumzia zoezi la upandaji miti, amesema TRA imeamua kuhusisha maadhimisho hayo na shughuli za uhifadhi wa mazingira ili kuhamasisha jamii kutunza mazingira na kuchangia juhudi za kitaifa za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia amewahimiza Watanzania kuendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa kwa kudai risiti za kielektroniki wanaponunua bidhaa au huduma na kutoa risiti wanapouza bidhaa au huduma, akisisitiza kuwa ulipaji wa kodi ni msingi wa maendeleo na utoaji wa huduma bora za kijamii kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Miyuji B, Mwalimu Joshua Nashari, ameishukuru TRA Mkoa wa Dodoma kwa kuichagua shule hiyo kwa zoezi la upandaji miti, akieleza kuwa miti hiyo itachangia kuboresha mazingira ya shule na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutunza mazingira.

Baadhi ya wazazi waliohudhuria shughuli hiyo, wameahidi kuwa wataendelea kushirikiana na walimu pamoja na wanafunzi kuitunza miti hiyo ili ikue na kuendelea kutoa manufaa kwa shule na jamii kwa ujumla kwa miaka mingi ijayo.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...