Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amewapongeza waandishi wa habari nchini kwa kazi wanayoifanya ya kuhabarisha umma, akieleza kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi.
Msigwa ameyazungumza hayo leo katika Mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma ambapo amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi, akisisitiza kuwa bila vyombo vya habari na waandishi wake, mawasiliano kati ya Serikali na wananchi yasingekuwa na ufanisi unaostahili.
"Mnafanya kazi nzuri sana na ya kizalendo kwa maslahi ya Tanzania. Serikali inatambua jukumu lenu na itaendelea kushirikiana nanyi wakati wote mtakapohitaji ushirikiano," amesema Msigwa.
Amesema Serikali itaendelea kuipa ushirikiano sekta ya habari kwa kuwa inaamini waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kujenga jamii yenye taarifa sahihi, uwajibikaji na maendeleo.
Hata hivyo, Msigwa amesema bado wapo watu wanaotamani kuona waandishi wa habari wakitumiwa kusambaza maudhui yanayoweza kuleta madhara kwa jamii na taifa, ikiwemo taarifa za uongo, chuki, uchonganishi, udhalilishaji pamoja na maudhui yanayolenga kuidhalilisha Tanzania.
Kwa mujibu wa Msigwa, hatua ya waandishi wengi wa habari kuendelea kusimamia misingi ya taaluma yao na kutokubali kutumiwa vibaya ni jambo la kupongezwa kwani limeendelea kulinda maslahi ya taifa na kuimarisha amani na mshikamano wa Watanzania.
Akizungumza kwa nafasi yake kama Msemaji Mkuu wa Serikali na msimamizi wa sekta ya habari nchini, Msigwa ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuzingatia maadili ya taaluma pamoja na sheria za nchi, huku wakitanguliza maslahi ya Watanzania katika kazi zao.
"Endeleeni kutumia kalamu zenu kwa manufaa ya Watanzania na maendeleo ya Taifa, si kwa maslahi ya watu wachache waliojipa jukumu la kuvuruga amani, umoja na mshikamano wa nchi," amesisitiza.
Kauli hiyo inaakisi msimamo wa Serikali wa kuendelea kushirikiana na sekta ya habari katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, zenye kujenga umoja wa kitaifa na kuchochea maendeleo ya Tanzania.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...