Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuandika historia mpya Julai 1, 2026 kwa kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kutoa Tuzo Maalum za Rais kwa Walipakodi Bora kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 9, 2026 kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo, amesema maadhimisho hayo yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo; “Miongo Mitatu ya TRA, Mlipakodi Shujaa, Tanzania Inayojitegemea.”
Kayombo ameeleza kuwa maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali za kitaifa na kikanda zitakazoanza kabla ya kilele chake Julai 1, 2026, kwa lengo la kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kuboresha huduma kwa walipakodi na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
Amefafanua kuwa shughuli hizo zitahusisha vipindi maalum vya elimu ya kodi kupitia redio, televisheni na majukwaa ya kidijitali, kliniki za kodi, huduma za ushauri kwa walipakodi, mikutano na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wahasibu na washauri wa kodi pamoja na ziara za kuwafikia walipakodi katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, maadhimisho hayo yataenda sambamba na utoaji wa Tuzo ya Rais kwa Walipakodi Bora, hatua inayolenga kutambua na kuthamini mchango wa walipakodi walioonyesha uadilifu, uwajibikaji na uzalendo katika kulipa kodi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa Kayombo, tuzo hizo zinalenga kuimarisha utamaduni wa ulipaji kodi na kutuma ujumbe kwamba kulipa kodi si wajibu wa kisheria pekee, bali ni kitendo cha uzalendo na ushiriki wa moja kwa moja katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara, huduma bora za kijamii na fursa zaidi kwa wananchi.
Ikumbukwe TRA ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge mwaka 1995 na kuanza rasmi shughuli zake Julai 1, 1996, ikiwa na jukumu la kusimamia ukusanyaji wa kodi na mapato mengine ya Serikali Kuu, kuwezesha ulipaji kodi kwa hiari na kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.
Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miongo mitatu na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha mchango wa kodi katika maendeleo ya Tanzania.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...