Na Janeth Raphael, MichuziTv
Watanzania wanatarajia kupata burudani ya hali ya juu ya soka la kimataifa baada ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutangaza rasmi kuwa litarusha mubashara Michuano ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 bila malipo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 9, 2026 jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Upendo Mbelle, amesema shirika hilo limefanikiwa kupata haki rasmi za kurusha mashindano hayo makubwa ya dunia yatakayofanyika kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, 2026 katika mataifa ya Marekani, Mexico na Canada.
Amesema Watanzania wataweza kufuatilia mashindano hayo kupitia televisheni ya TBC, redio, pamoja na majukwaa ya mtandaoni ikiwemo Facebook, YouTube, Instagram na TikTok, sambamba na tovuti rasmi ya shirika hilo.
“Tumejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata matangazo ya ubora wa juu, yakiambatana na uchambuzi wa kina kutoka kwa wachambuzi wenye uzoefu mkubwa wa soka,” amesema Mbelle.
Ameongeza kuwa uzoefu wa muda mrefu wa TBC katika kurusha matukio makubwa ya michezo, tangu enzi za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), umeiwezesha shirika hilo kuendelea kutoa huduma bora kwa watazamaji na wasikilizaji wake.
Kwa mujibu wa Mbelle, mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 utapigwa Juni 11, 2026, ukiwakutanisha wenyeji Mexico dhidi ya Afrika Kusini, ambapo TBC itakuwa tayari kuurusha mubashara kuanzia dakika ya kwanza.
Aidha, amesema TBC imeweka kaulimbiu maalum ya “Pira Mtelezo”, ikilenga kuwaletea Watanzania burudani ya kipekee ya soka la kimataifa wakiwa majumbani au walipo popote.
Upendo Mbelle amesisitiza kuwa TBC imewahi kurusha pia matoleo ya Kombe la Dunia ya mwaka 2010 Afrika Kusini, 2014 Brazil, 2018 Urusi na 2022 Qatar, jambo linaloonyesha uzoefu wake mkubwa katika utangazaji wa mashindano ya kimataifa.
Pia amebainisha kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, TBC imeendelea kuimarisha uwezo wake kupitia kurusha michuano mikubwa kama CHAN 2025 iliyofanyika Tanzania, Kenya na Uganda pamoja na AFCON 2025 iliyofanyika Morocco.
“Tunaendelea kujipanga kuhakikisha kila Mtanzania anapata nafasi ya kushuhudia soka la kiwango cha juu duniani kupitia chombo chake cha habari anachokiamini,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa TBC, Daphrosa Kimbory, amesema shirika hilo limejipanga kikamilifu kulinda haki zake za matangazo, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka makubaliano ya haki miliki.
Naye Mkuu wa Dawati la Michezo TBC, Evance Muhando, amesema TBC inaendelea kuwa nyumbani kwa wachambuzi na watangazaji wengi wa soka nchini, na amewakaribisha Watanzania kufurahia mashindano hayo mubashara kupitia chombo hicho cha umma.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...