Na Janeth Raphael MichuziTv 

Serikali imewataka wakulima na wadau wote wa zao la pareto nchini kuweka mkazo katika uzalishaji wenye ubora ili kuongeza ushindani wa zao hilo kwenye soko la kimataifa na kuinua mchango wake katika uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 16 wa Wadau wa Zao la Pareto uliofanyika Juni 26, 2026, jijini Dodoma

Silinde amesema maendeleo ya sekta ya pareto yanategemea uzalishaji unaokidhi viwango vya ubora, huku akisisitiza wadau kutumia mkutano huo kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji kutoka tani 3,800 zilizozalishwa mwaka 2025/2026 hadi kufikia lengo la tani 9,000 kwa mwaka.

Aidha, amewataka wadau kuboresha ubora wa maua ya pareto kwa kuzingatia viwango vinavyohitajika sokoni, ikiwemo kuongeza kiwango cha kirutubisho cha asili cha pyrethrin, ambacho ndicho kinacholipa thamani kubwa zao hilo katika biashara ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Silinde, pareto ni moja ya mazao ya kimkakati yanayoendelea kuingizia Tanzania fedha za kigeni, ambapo kwa sasa mauzo yake nje ya nchi yanaingiza takribani Dola za Marekani milioni 9, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 23.4 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, amesema mamlaka hiyo tayari imeanza kusambaza vifaa vya kudhibiti unyevu wa pareto katika halmashauri 17 zinazolima zao hilo, hatua inayolenga kulinda ubora wa mazao baada ya kuvunwa.

Ameongeza kuwa katika kipindi kifupi kijacho, COPRA itaanza ujenzi wa vituo vya kukaushia pareto ili kupunguza upotevu wa ubora na kuongeza thamani ya zao hilo kabla ya kuingia sokoni.

Mlola amesema mkutano huo pia unajadili namna ya kuwashirikisha vijana zaidi katika mnyororo wa thamani wa pareto kupitia uzalishaji wa mbegu bora, shughuli za ugani, usindikaji pamoja na maeneo mengine ya biashara yanayohusiana na zao hilo.

Mkutano huo umehudhuriwa na wakulima wa pareto kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakurugenzi wa halmashauri zinazozalisha zao hilo, viongozi wa serikali, maafisa ugani pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo.

Katika hafla hiyo, Naibu Waziri David Silinde alimwakilisha Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ambaye alikuwa na majukumu mengine ya kitaifa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...