-Wanaume 14 tayari mambo yao safi, daktari aeleza hatua zote muhimu


Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma


HOSPITALI ya Benjamin Mkapa imesema gharama za huduma ya upandikizaji wa uume katika hospitali hiyo ni Sh.milioni 10, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusaidia wanaume wenye changamoto za kiafya zinazohusiana na nguvu za kiume kurejesha furaha ya ndoa.

Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea hospitali hiyo na kushuhudia mafanikio lukuki ya utoaji huduma, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dkt. Abdallah Baja amesema huduma ya kupandikiza uume inafanyika katika hospitalini hapo peke yake.

“Tumekuwa tukitoa huduma hii ya kupandikiza uume tangu mwaka 2023 na huduma hii ni sehemu ya huduma za kibingwa na kibingwa bobezi tunazozitoa zaidi ya 20.”

Amefafanua hospitali hiyo iliamua kuanzisha huduma hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto kubwa miongoni mwa wanaume wengi, hali iliyosababisha baadhi yao kutafuta suluhisho kupitia waganga wa kienyeji na dawa zinazodaiwa kutibu tatizo hilo.

“Tuliona umuhimu wa kuja na mkakati wa kuwasaidia watu wenye changamoto za nguvu za kiume. Kwa maana hiyo, tulianza kutoa huduma hii na hadi sasa wanaume 14 wamepandikizwa uume.”

Ameongeza baada ya kufanyiwa matibabu hayo, wanaume hao walitoa mrejesho mzuri kuhusu hali zao na kwamba walipewa maelekezo ya kuanza kushiriki tendo la ndoa baada ya wiki sita tangu kufanyiwa upasuaji.

“Hizo ni taarifa kutoka kwao wenyewe kwa sababu tuliendelea kuwafuatilia. Wametueleza kuwa hali zao ni nzuri na wamefurahi kwa kuwa uwezo wao umerudi, jambo ambalo limewarejeshea heshima katika familia zao,” amesema Dkt. Baja.

Ameongeza kwamba hospitali hiyo ipo katika mkakati wa kupanua huduma hiyo ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitaji matibabu hayo.

“Kinachofanyika si kuweka uume bandia bali uume wako tupandikiza vitu vya kuamsha msuli na baada ya kufanyiwa upasuaji unarudi katika hali yako ya kawaida na unakuwa hadi mwisho wa uhai wako,” amesema.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...