Na Mwandishi Wetu
UJUMBE wa walimu na viongozi wa elimu kutoka Mkoa wa Dodoma wapatao 40 umeondoka kwenda Korea Kusini kujifunza mbinu za kisasa za ufundishaji, usimamizi wa shule na matumizi ya teknolojia katika elimu.

Walimu hao wanatarajiwa kushiriki mafunzo na ziara ya kielimu ya siku nne ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi mkoani humo.

Mratibu wa safari hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, amesema walimu hao waliondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuelekea Seoul, Korea Kusini, kupitia Doha, Qatar.

Amesema katika ziara hiyo washiriki watajifunza namna Korea Kusini inavyotumia teknolojia, ubunifu, nidhamu na usimamizi bora katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji. Pia watapata uzoefu kuhusu matumizi ya mifumo ya kidijitali darasani, maandalizi ya masomo na ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi.

Amesema kabla ya kuondoka walipatiwa mafunzo ya maandalizi kuhusu utamaduni wa Korea Kusini, utunzaji wa muda na wajibu wao kama wawakilishi wa Mkoa wa Dodoma na Tanzania.

Amesema lengo la safari hiyo si kutembelea Korea Kusini pekee, bali kujifunza uzoefu wa kimataifa utakaosaidia kuboresha ufundishaji, usimamizi wa shule na kuongeza ufaulu wa wanafunzi watakaporejea nchini.

Amesema mpango huo umetokana na jitihada za Mkoa wa Dodoma za kutambua na kuwapa motisha walimu walioonesha utendaji bora, baada ya Mkutano wa Wadau wa Elimu uliowakutanisha viongozi wa Serikali, walimu, maofisa elimu, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ya elimu.

Amesema safari hiyo imefanikishwa kupitia ushirikiano wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali, wakiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Benki ya NMB na Global Education Link, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza maendeleo ya kitaaluma kwa walimu na kuboresha sekta ya elimu.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...