Zaidi ya wananchi 300 wametembelea banda la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) tangu kuanza kwa Wiki ya Utumishi wa Umma, wakipata elimu na ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara katika maeneo yao, hatua hiyo imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na taasisi hiyo huku ikitoa fursa ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi moja kwa moja.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa TARURA, Catherine Sungura, amesema wananchi wanaowasilisha kero zao huunganishwa moja kwa moja na mameneja wa maeneo husika ili kupata maelezo ya kina pamoja na ufumbuzi wa haraka, ameeleza lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi inayotekelezwa na maendeleo yake.
Katika mwendelezo wa Wiki ya Utumishi wa Umma unaoendelea Jijini Dodoma hadi Juni 23, Sungura alieleza kuwa mwananchi kutoka eneo la Kimara amewasilisha maswali kuhusu maendeleo ya miundombinu ya barabara katika eneo lao , amesema TARURA imekuwa ikitoa ufafanuzi wa kina kwa kila mwananchi anayefika kwenye banda hilo.
Akizungumzia barabara ya King'ong'o iliyopo Kimara, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Sungura amesema ujenzi wa barabara ya zege unaoanzia eneo la TRA kuelekea King'ong'o unaendelea vizuri, amebainisha kuwa amewasiliana na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ubungo na amewahakikishia wananchi kuwa kilomita 1.6 pekee ndizo zimebaki kukamilishwa, huku mita 800 zikitarajiwa kujengwa mwanzoni mwa mwaka mpya wa fedha kuanzia Julai na sehemu iliyobaki kukamilishwa katika awamu inayofuata.
Amesisitiza kuwa TARURA itaendelea kuhakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa ili kurahisisha mawasiliano na usafiri kwa wananchi, huku akieleza kuwa barabara bora zinachochea upatikanaji wa huduma za kijamii, biashara na shughuli nyingine za maendeleo jambo ambalo ni muhimu katika kuinua ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa maeneo mbalimbali nchini.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...