Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu alama za kiusalama zilizopo kwenye noti za Tanzania ili kuwawezesha kutambua tofauti kati ya Sarafu halali na bandia, sambamba na kuhamasisha utunzaji sahihi wa fedha ili zisiharibike au kuchakaa mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 4, 2026, Afisa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sarafu BoT, Shadrack Mapunda, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuandaa mahitaji ya sarafu, kuzitengeneza na kuhakikisha zinapatikana kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uchumi.

Mapunda amesema upangaji wa mahitaji ya fedha huzingatia mambo mbalimbali ikiwemo kasi ya ukuaji wa uchumi, ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya utengenezaji wa sarafu, ameongeza kuwa BoT huhifadhi noti na sarafu zilizotengenezwa katika maghala maalumu yaliyopo kwenye ofisi zake saba nchini pamoja na vituo vidogo vya kusambazia fedha kwa kushirikiana na benki za biashara kwenye maeneo ambayo hawana ofisi.

Aidha, amesema BoT imekuwa ikiendesha kampeni za elimu kwa umma kuhusu alama za kiusalama zilizopo kwenye sarafu za Tanzania ili wananchi waweze kuzitambua kwa urahisi na kuepuka kupokea noti bandia katika shughuli zao za kila siku.

Mapunda amesisitiza kuwa sheria za nchi zinakataza mtu yeyote kuharibu sarafu kwa makusudi, akieleza kuwa anayebainika kufanya kitendo hicho anakuwa ametenda kosa na ataadhibiwa kwa kifungo kisichopungua miezi sita, au faini ya kuanzia shilingi 500,000, au adhabu zote mbili kulingana na uamuzi wa mahakama.

Pia amewahimiza wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika kwenye ofisi za Benki Kuu ya Tanzania ili kupata elimu zaidi kuhusu sarafu za Tanzania, alama zake za kiusalama pamoja na majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Benki kuu ya Tanzania (BoT).


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...