Jane Mwakyoma - Rukwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Missana Kwangura amehitimisha mafunzo ya utoaji wa elimu kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika wilayani humo mkoani Rukwa.

Kwangura aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga  Nyakia Chirukile kama mgeni rasmi amesema mafunzo hayo yanapaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa washiriki na jamii kwa ujumla kwa kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha shughuli zao za kiuchumi.

"Kupitia mafunzo haya mliyoyapata, hakikisheni yanakuwa chachu ya maendeleo katika jamii. Tumiaeni maarifa haya kuongeza thamani ya shughuli zenu za kiuchumi, kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya Taifa," alisema  Kwangura.

Aidha amesema programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi zina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi, kupunguza umaskini na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa Jacqueline Chrisant Mzindakaya amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wananchi uwezo wa kutambua na kunufaika na fursa mbalimbali za mitaji ili waweze kuanzisha, kuendeleza na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Gwakisa Bapala amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa NEEC wa kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu fursa za mitaji, namna ya kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili pamoja na matumizi sahihi ya mikopo ili kukuza biashara.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, wakiwemo SELF Microfinance Fund (SELF MF), Benki ya CRDB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Agricultural Inputs Trust Fund (AGITF), Azania Bank pamoja na PASS Trust, ambao wametoa elimu kuhusu huduma na fursa za kifedha zinazopatikana kwa wananchi .




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...