Pendekezo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) la kuongeza bei ya maji kwa matumizi ya nyumbani kutoka shilingi 1,730 hadi shilingi 2,700 kwa kila mita ya ujazo limejadiliwa katika mkutano wa wadau ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) uliofanyika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Mkutano huo umefanyika Julai 16, 2026, ukiwa na lengo la kukusanya maoni ya wananchi na wadau kuhusu ombi hilo la marekebisho ya bei za huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31.

Akifungua mkutano huo, Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa EWURA, Mhandisi Walter Christopher, amesema zoezi hilo ni sehemu ya utaratibu wa kisheria unaolenga kuhakikisha maamuzi ya bei yanafanywa kwa kuzingatia maoni ya wananchi pamoja na hali halisi ya utoaji wa huduma.

Mhandisi Christopher amesema SOUWASA imeomba marekebisho ya bei kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na matengenezo, upanuzi wa mtandao wa maji na majitaka pamoja na ukarabati wa miundombinu chakavu.

Ameeleza kuwa EWURA itachambua maoni yote yatakayopokelewa kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, huku akisisitiza kuwa lengo ni kupata uwiano kati ya uwezo wa wananchi kumudu gharama za maji na uwezo wa mamlaka kuendelea kutoa huduma bora na endelevu.

Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema sekta ya maji ni msingi wa maendeleo ya jamii na uchumi, hivyo maamuzi kuhusu bei yanapaswa kufanyika kwa ushirikishwaji wa wananchi.

Kwa upande wake, Mhandisi Jafari Kinjalambaya wa SOUWASA amesema mapendekezo ya marekebisho ya bei yanalenga kuwezesha mamlaka kukarabati kilomita 32 za mabomba chakavu, kujenga vyanzo vipya vya maji, matenki na mtambo wa kutibu maji, kusambaza mabomba kwa urefu wa kilomita 194.7, kupanua mtandao wa majitaka kwa kilomita 14 pamoja na kufunga mita mpya za malipo ya awali na kubadilisha mita chakavu ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na huduma kwa wateja.

Hata hivyo, wananchi na viongozi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo wametoa maoni tofauti kuhusu pendekezo hilo, wakitaka Serikali na EWURA kuzingatia uwezo wa wananchi wenye kipato cha chini kabla ya kuidhinisha ongezeko la bei.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...