Na Mwandishi wetu, Mirerani
MWENGE wa uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, iliyojengwa na kampuni ya Chusa Mining LTD.
Kampuni ya Chusa Mining LTD chini ya Mkurugenzi wake Joseph Damasi Mwakipesile imejenga wodi hiyo ya wanawake na watoto kwa gharama ya shilingi milioni 230 kupitia mchango wao kwa jamii (CSR).
Kiongozi wa mbio za mwenye wa uhuru kitaifa mwaka 2026 Wazo Mwang'onda ameipongeza Chusa Mining LTD kwa kujenga wodi hiyo ambayo wanawake na watoto watalazwa na kupata huduma za afya katika kituo hicho cha afya pindi wakiugua.
Amesema mdau huyo wa maendeleo amejenga jengo hilo kutokana na jitihada za dhati za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kuweka mazingira rafiki kwa wachimbaji kufanya kazi, nao kutoa kiasi kwa jamii.
"Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwa sisi wakristo tunaamini kuwa Mungu anakujaribu pale unapotoa kwani amesema nijaribuni kupitia majitoleo na atakubariki pale ulipotoa hongera sana mdau wa maendeleo kwa kujitolea," amesema Mwang'onda.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya ambaye pia ni Mbunge wa Simanjiro amesema hatua ya Chusa Mining LTD kuwjenga wodi hiyo ni maendeleo makubwa.
Ole Millya amesema Chusa Mining wamekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwani wanakwenda kumaliza changamoto ya upungufu ya wodi ya kulaza wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa kampuni ya Chusa Mining LTD, Joseph Mwakipesile ametoa shukrani kwa Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa namna wanavyotoa ushirikiano katika kazi zao.
Mwakipesile amesema wamejenga jengo hilo baada ya kusikia changamoto ya wodi ya wanawake na watoto ili kurudisha kidogo wanachokipata kwa jamii.
"Tunashukuru leo hii mwenge wa uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye mradi huu wa wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani," amesema Mwakipesile.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani Dkt Namnyaki Lukumay akisoma taarifa ya mradi huo amesema umegharimu shilingi milioni 230 na kujengwa na kampuni ya Chusa mining LTD.
Dkt Namnyaki amesema lengo kuu la mradi huo ni kuboresha upatikanaji wa huduma bora na rafiki za afya kwa wanawake na watoto na kuboresha afya ya familia na jamii kwa ujumla.
Amesema mradi huo ukikamilika utahudumia wanawake 5,000 na watoto zaidi ya 7,000 kwa mwaka katika kituo cha afya cha Mirerani.
"Sisi wananchi wa Simanjiro tunaishukuru Serikali ya awamu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya, kwa heshima na taadhima tunaomba utembee, kukagua na kuweka jiwe la msingi mradi wetu wa jengo la msingi mradi wetu wa jengo la wodi ya wanawake na watoto katika kituo cha afya Mirerani," amesema.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...