Na Mwandishi wetu, Babati

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege amekabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hospitali ya Dareda Mission ya wilaya ya Babati mkoani Manyara, yenye ukosefu wa uzio, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wagonjwa na mali za hospitali.

Hatua hiyo imekuja kufuatia changamoto hiyo, ambapo Naibu Waziri Ndege aliahidi kuhakikisha uzio wa hospitali hiyo unajengwa kwa haraka ili kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya na kuongeza usalama kwa wagonjwa, watumishi na jamii wanaofika kupata huduma.

Naibu Waziri Ndege amesema huo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa uongozi na watumishi wa hospitali kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) mwaka huu, baada ya kubaini ukosefu wa uzio ulikuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili hospitali hiyo.

"Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya nchini ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vyema katika mazingira salama na rafiki," amesema Naibu Waziri Ndege.

Amesisitiza wadau pamoja na wananchi kuendelea kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa na serikali ili ijengwe kwa viwango vinavyotakiwa na kuhakikisha thamani ya fedha zinazotolewa na serikali.

Ameeleza kuwa kuboresha miundombinu ya hospitali ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha mazingira ya utoaji wa huduma za afya yanakuwa bora, salama na yenye kukidhi mahitaji ya watu.

Pia, Naibu Waziri Ndege amewahakikishia viongozi wa hospitali ya Dareda Mission kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kuboresha miundombinu ya hospitali hiyo kwa maslahi ya jamii.

Mkurugenzi wa hospitali ya Dareda Mission, Padri Peter Salaho, ameishukuru serikali kwa mchango huo mkubwa, akisema utasaidia kuimarisha usalama wa hospitali na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma zake.

"Tunakushukuru sana Naibu Waziri Ndege, kwani ulipotembelea hospitali yetu tulikueleza changamoto ya ukosefu wa uzio na ulituahidi kutusaidia, sasa umetimiza ahadi yako," amesema Padri Salaho.

Diwani wa kata ya Dareda, Willbrod Bayo amempongeza na kumshukuru Naibu Waziri Ndege kwa kutimiza ahadi yake ya kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa hospitali hiyo.

"Mara zote Naibu Waziri Ndege umekuwa msaada mkubwa kwa jamii, taasisi binafsi, za umma na mashirika ya kidini, tunakushukuru mno kwa kujitolea kwako kila wakati ukiitwa unaitika," amesema Bayo.

Mkazi wa Dareda kati Aloyce Tluway amempongeza Naibu Waziri Ndege kwa kutoa mifuko hiyo ya saruji ili kujenga ukuta kwani hospitali hiyo inaheshima kubwa kwa jamii ya eneo hilo.

"Hospitali ya Dareda Mission ni kongwe, watu wengi wamepata huduma hapo wengine wamezaliiwa hapo, wapo waliotibiwa maleria au kufanyiwa upasuaji hivyo Naibu Waziri Ndege amefanya jambo jema sawa na kulipa wema kwa jamii," amesema Tluway.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...