Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, huduma mbalimbali na umuhimu wa ithibati katika kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari nchini.
Hatua hiyo imejidhihirisha leo baada ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, kuungana na maafisa wa Bodi katika banda la JAB lililopo Kijiji cha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kutoa elimu kwa wananchi, kujibu maswali mbalimbali na kuzungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda hilo.


Akizungumza katika maonesho hayo, Wakili Kipangula alisema JAB imejipanga kuhakikisha wananchi na wadau wa sekta ya habari wanapata uelewa sahihi kuhusu majukumu ya Bodi pamoja na huduma zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari.
Alisema ushiriki wa JAB katika maonesho ya Sabasaba unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi, kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa ithibati kwa waandishi wa habari na kuhamasisha uzingatiaji wa maadili, weledi na uwajibikaji katika taaluma ya uandishi wa habari.
Mbali na kutoa elimu, JAB inaendelea kutoa huduma mbalimbali katika banda lake ikiwemo usajili wa waandishi wa habari, utoaji wa vitambulisho vya ithibati kwa waliokidhi vigezo, marekebisho ya taarifa za usajili pamoja na ushauri kuhusu huduma zinazotolewa na Bodi.
JAB imewahimiza waandishi wa habari, wadau wa sekta hiyo na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya Maonesho ya Sabasaba kutembelea banda lake ili kupata huduma, elimu na ufafanuzi kuhusu shughuli zake, huku ikisisitiza kuwa ithibati ni nyenzo muhimu katika kujenga taaluma ya uandishi wa habari yenye weledi, uwajibikaji na kuaminika.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...