Na Janeth Raphael MichuziTv 

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameelezwa kuwa moja ya majukwaa makubwa yanayochochea ukuaji wa biashara, uwekezaji na ubunifu nchini, huku yakiiunganisha Tanzania na masoko ya kikanda pamoja na ya kimataifa.

Akizungumza katika ufunguzi rasmi Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam leo, Ijumaa Julai 3, 2026, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema maonesho hayo yameendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya sekta ya biashara kwa kipindi cha nusu karne.

Rais Samia amesema Sabasaba imekuwa jukwaa linalowakutanisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi, jambo ambalo limeongeza fursa za biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Amebainisha kuwa mafanikio ya maonesho hayo yanaonekana kupitia wafanyabiashara wengi walioanza safari zao kwa mitaji midogo wakitumia Sabasaba kutangaza bidhaa na huduma zao, lakini sasa wamekua na kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wanaochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.

Aidha, amesema maonesho hayo yameendelea kuwa chanzo cha manufaa kwa wakulima, wajasiriamali na wabunifu kwa kuwapatia nafasi ya kutafuta masoko mapya, kujifunza teknolojia na mbinu za kisasa za uzalishaji, pamoja na kupata washirika na mitaji ya kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Rais Samia, Sabasaba imeendelea kuijengea Tanzania taswira nzuri kama kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, huku pia ikifungua milango ya masoko katika Bara la Afrika na sehemu nyingine duniani.

Ametoa wito kwa waandaaji wa maonesho hayo pamoja na wadau wa sekta binafsi kuendelea kubuni mbinu mpya zitakazoyawezesha Maonesho ya Sabasaba kufikia viwango vya kimataifa, ili yaendelee kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo ya biashara nchini.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...