Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameiomba Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya marejeo yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akidai hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuchelewesha usikilizwaji wa kesi ya tuhuma za uhaini inayomkabili.
Lissu alidai hayo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani baada ya Jamhuri kufungua shauri la mapitio kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali notisi ya Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Alidai uamuzi wa Mahakama Kuu wa Februari 24, 2026 haukumaliza kesi ya msingi ya uhaini, hivyo ni uamuzi mdogo usioruhusiwa kukatiwa rufaa wala kuwasilishwa maombi ya marejeo kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Rufani.
Lissu pia alidai DPP hakupaswa kuwasilisha maombi hayo moja kwa moja Mahakama ya Rufani bali alitakiwa kwanza kuandika barua rasmi kwa Jaji Mkuu.
Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga na Job Mrema waliieleza Mahakama kuwa Lissu ametegemea kanuni za mashauri ya madai badala ya jinai na kwamba maombi ya DPP yamewasilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Rufani na Kanuni zake.
Katuga alidai Mahakama Kuu ilikataa ushahidi huo kabla haujapokelewa na kupimwa, jambo ambalo lilinyima Jamhuri haki ya kusikilizwa kikamilifu, huku akisisitiza kuwa Mahakama ilipaswa kuangalia uhalali wa notisi ya kuongeza ushahidi.
Mrema naye alidai pingamizi la awali la Lissu halina uwezo wa kuondoa shauri lote na kwamba halijazingatia sheria ya sasa kwa kuwa linahusu mashauri ya madai.
Katika majibu yake, Lissu aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi hayo na iamuru DPP amlipe fidia kwa kile alichodai ni ucheleweshaji wa makusudi wa shauri lake, akisema amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na miezi mitatu huku kesi ikicheleweshwa kwa siku 139.
Katuga alipinga madai hayo akieleza kuwa maombi hayo hayajalenga kuchelewesha kesi na kwamba Mahakama ya Rufani ina mamlaka ya kuhakikisha mwenendo wa Mahakama Kuu unafuata sheria.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama iliahirisha shauri hilo hadi itakapotoa uamuzi wake kwa tarehe ambayo pande zote zitajulishwa.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...