TANZANIA imeendelea kupiga hatua katika sekta ya afya baada ya kuanza kutumika kwa kipimo kipya cha Checkfor UTI Test, kinachomwezesha mtu kujipima akiwa nyumbani ili kubaini uwezekano wa maambukizi ya njia ya mkojo (UTI).
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Dkt. Eshton Nkala alisema maambukizi ya UTI ni miongoni mwa changamoto za kiafya zinazowakumba watu wengi, huku dalili zake zikijumuisha kukojoa mara kwa mara, maumivu au muwasho wakati wa kukojoa, maumivu ya chini ya tumbo na mkojo kubadilika rangi au kuwa na harufu isiyo ya kawaida.
Alisema changamoto kubwa imekuwa ni kuchelewa kutambua dalili na kufika katika vituo vya afya, wakati utambuzi wa mapema husaidia kupunguza uwezekano wa maambukizi kuongezeka, kujirudia au kusababisha madhara zaidi kiafya.
Kwa mujibu wake, Checkfor UTI Test humsaidia mtu kupata taarifa za awali kuhusu uwezekano wa kuwa na UTI akiwa nyumbani, lakini hakichukui nafasi ya daktari wala hospitali, bali humwezesha mtumiaji kuchukua hatua mapema na kufika kituo cha afya kwa ushauri wa kitaalamu, vipimo zaidi na matibabu stahiki.
Dkt. Nkala alisema kipimo hicho kinazalishwa nchini na kampuni ya Canadian Biotech, hatua inayoonyesha mchango wa viwanda vya ndani katika uzalishaji wa vifaa tiba vinavyosaidia jamii kujitambua mapema na kuchukua hatua kwa wakati.
Aliongeza kuwa Checkfor UTI Test kinapatikana kupitia JD Pharmacy, Bariki Pharmacy na Cugra General Supplier, huku akisisitiza kuwa wananchi hawapaswi kupuuza dalili za UTI, bali wajitambue mapema na kutafuta matibabu sahihi kwa wakati.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...