Na. Saidina Msangi, WF, Abidjan.

Nchi za Afrika zimekubaliana kuweka kipaumbele katika ufadhili wa viwanda vinavyotegemea rasilimali za ndani ikiwemo madini na kuhakikisha kuwa zinaongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha biashara ya ndani ya bara ili kujenga maendeleo jumuishi, endelevu na yenye tija.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, uliofanyika jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.

Mhe. Munde alisema hatua hiyo inalenga kuharakisha mageuzi ya uchumi kwa kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo, kuimarisha ushirikiano wa kikanda ili kupunguza utegemezi kutoka kwa wafadhili.

‘‘Afrika ina utajiri mkubwa wa madini, biashara na utalii ambazo ni nguzo kuu zinazoweza kukuza uchumi kama kutawekwa uratibu mzuri na madhubuti baina ya mataifa wanachama, na kuweka mikakati ya kusimamia ustahimilivu wa madeni ya taifa ili kupunguza utegemezi wa kifedha kutoka kwa wadau wa nje’’, alisema Mhe. Munde.

Aidha, Mhe. Munde alisema Afrika ina nguvu kazi ya vijana wenye ubunifu na nguvu ambapo wakiwezeshwa kupitia uboreshaji wa mifumo ya elimu na mafunzo ya ujuzi, pamoja na kuweka mazingira ya kutumia teknolojia mpya na za kisasa kama Akili unde (AI) itawezesha kuwa na nguvu kazi yenye ushindani wa kimataifa na kuchochea mapinduzi ya viwanda na kiuchumi barani Afrika.

‘‘Katika kukuza biashara ya kikanda, tulijadili umuhimu wa kuondoa vikwazo vyote vya ushuru na visivyo vya ushuru, kufanyia marekebisho sheria na sera za nchi zilizokuwa zikibagua wafanyabiashara wa Afrika pamoja na kuimarisha na kujenga shoroba mpya za kiuchumi zitakazounganisha nchi na nchi, ili kuwezesha mzunguko huru wa watu, bidhaa, na huduma kupitia Eneo la Biashara Huru la Afrika (AfCFTA)’’, alifafanua Mhe. Munde.

Awali akizungumza wakati akichangia mada, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, alisema ili kuharakisha mageuzi ya kiuchumi Afrika ni muhimu kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kuendeleza shoroba za kiuchumi, pamoja na kuweka mifumo bora ya usafirishaji na ugavi ili kuongeza ushindani katika masoko ya kikanda na ya kimataifa.

‘‘Ili kufikia azma hii, ni lazima kuratibu sera za udhibiti na kushughulikia vikwazo vya biashara ya mipakani, ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, uhuru wa watu kusafiri, na kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu kama vile barabara, reli, bandari na njia za maji ili kuunganisha nchi zetu na kurahisisha mwingiliano wa watu, bidhaa na huduma’’, alisema Mhe. Londo.

Alisisitiza kuwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na madini na vituo vya uchakataji, Afrika itaweza kujenga minyororo imara ya thamani ya kikanda na kuongeza mauzo ya bidhaa zilizochakatwa zenye kukidhi viwango vya kimataifa, badala ya kuendelea kuuza malighafi pekee.

Mkutano huo uliofanyika kwa siku mbili uliokuwa na kaulimbiu "Kufadhili Maendeleo ya Viwanda barani Afrika kwa Maendeleo Endelevu" (Financing Africa's Industrialization for Sustainable Development), ulilenga kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda vinavyotegemea rasilimali za madini barani Afrika.


Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiagana na Waziri wa Maliasili na Nishati wa Eswatini ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, Mhe. Prince Damian, baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.




Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akiongoza Mkutano kuthibitisha maazimio ya kikao, katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.


Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Dennis L. Londo, akichangia mada katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.








Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, akichangia mada katika Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.


Naibu Waziri wa Fedha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akipongezwa na Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Dennis Londo, (kulia), na Naibu Katibu Mkuu Mtendaji, Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Blandina Kilama (wa pili kulia), baada ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Pamoja wa 9 wa Kamati Maalum ya Mawaziri (STC) ya Umoja wa Afrika inayosimamia masuala ya Fedha, Uchumi, Mipango na Mtangamano pamoja na Mkutano wa 5 wa Kamati Maalum ya Mawaziri inayosimamia masuala ya Biashara, Utalii, Viwanda na Madini, jijini Abidjan, nchini Côte d’Ivoire.




(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Abidjan, Côte d’Ivoire.)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...