Na Mwandishi Wetu

KAMPENI maalum ya Kuwa Makini Okoa Maisha kwa madereva bodaboda maarufu kama maofisa usafirishaji imeanza rasmi mkoani Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwapatia mafunzo ya elimu ya usalama barabarani pamoja na vifaa kinga kama sehemu ya kukomesha ajali za barabarani.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo leo Julai 25,2025 na maofisa usafirishaji katika eneo la Tangi Bovu -Kawe wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam Rais wa Chama cha Watalaam wa Afya na Usalama Mahala Pa kazi Tanzania(TOHASA) Caroline Baraza amesema wameamua kuja na kampeni hiyo ya kuwapatia elimu hiyo ya usalama barabarani ili kupunguza ajali.

“Lengo ni kuwapatia elimu maofisa usafirishaji ili wawe makini na kuheshimu sheria kwasababu tunaangalia ajali nyingi zinazotokea na takwimu zinaonesha watu wengi wanakosa elimu na kutokujua wafanye nini wakati gani lakini lengo kuu ni kuokoa maisha ndio maana hizi Reflecta zetu zimeandikwa kuwa makini okoa maisha hiyo ndio kauli mbiu yetu tunayokwenda nayo .

“Mwito wa TOHASA kwa maofisa usafirishaji wafuate sheria za barabarani kwani hazina mtu huyu na huyu bali ziko kwa ajili yetu sote tunaotumia barabara.Pia kuwa makini pale inapobidi unapoona mwenzako anavunja sheria wewe kuwa makini na mfundishe au kumuekeleza.”

Amesema katika chama hicho wameshirikiana na wadau mbalili na wakiwemo OSHA WCF, Safety and Security, Jafferjee na TMHS group

Kwa upande wake Mkuu wa usalama barabarani Wilaya ya Polisi Kawe/Mbweni Mkoa wa Kinondoni Adrian Kamara amesema kupitia kampeni ya TOHASA wametoa elimu kwa maofisa usafrishaji katika kituo cha Tangi Bovu.

“Tumeshirikiana na TOHASA ambao wanahusika na usalama mahala pa kazi kuwakumbusha madereva pikipiki kuzingatia usalama na abiria pamoja na utumiaji sahihi wa barabara ,watii sheria za usalama barabarani kwa maana ya kuheshimu vivuko ,kutoendesha pembeni ya barabara.

“Tumewafahamisha wao ni watumiaji rasmi na wanatambulika kisheria hivyo waendeshe pikipiki zao katikati ambako ni sehemu sahihi kama ni kushoto au kulia kufuata utaratibu kama magari yanavyotembea kwani dereva makini hawezi kumparamia mwendesha pikipiki”

Pia amesema wamewasisitiza lakini uvaaji wa viakisi mwanga (Reflekta) ili waweze kuonekana nyakati za usiku au wanapoendesha katika maeneo yenye uono hafifu kwa madereva wengine wa barabara .Wamewakumbusha uvaaji kofia ngumu bila kujali umri lakini TOHASA imewapa reflecta viakisi mwanga pamoja na mawani kwa ajili ya kujikinga na vumbi.

Wakati huo huo Gerald Mrema ambaye ni Makamu wa Rais wa TOHASA amesema wameamua kufanya kampeni hiyo kwasababu kuna ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali za barabarani ,majeruhi pamoja na ulemavu wa kudumu hivyo wao wameamua kama taasisi ya usalama mahala pa kazi kujikita kuwapa elimu hiyo.

“Taasisi yetu kwa kushirikiana na Jeshi la

Polisi pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zinatoa vifaa kinga vya usalama pahala pa kazi tumetoa elimu kwa bodaboda tukiwa na kusudi kubwa baada ya elimu hii watahakikisha wanaendesha vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi kwa kufuata alama za barabarani kwa kutopakia abiria zaidi ya mmoja,”amesema Mrema.

Aidha amesisitiza umuhimu wa madereva bodaboda kuhakikisha wanavaa vifaa kinga wanapokuwa mahala pa kazi kwa mfano reflekta ili waonekane kwa mbali lakini kuvaa viatu kinga ambavyo ajali iwapo itatokea vitalinda miguu yao sambamba na utaratibu wa ukaguzi wa vyombo vyao vya moto mara kwa mara asubuhi kabla ya kuanza kutumia ili kuona kama chombo ni salama kwa ajili ya matumizi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tangi Bovu Shule Athuman Kitunguu amesema wanashukuru kwa kupatiwa elimu ya usalama barabarani pamoja na vifaa kinga huku akieleza kumekuwepo na changamoto nyingi ikiwemo ajali za barabarani na kwamba Jeshi la Polisi kupitia elimu wanazotoa sasa wanathaminiwa ikilinganishwa na hapo awali.

“Kwasasa tunashukuru Jeshi la Polisi limepoa na wanatupa ushirikiano mzuri na elimu ambazo tunapatiwa zinatuongezea uelewa kuhusu kuhusu kufuata sheria za usalama barabarani.”













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...