Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Katika kuimarisha juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, waandishi wa habari na maafisa mawasiliano Serikalini wamehimizwa kujenga ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu na utekelezaji wa kampeni zinazolenga kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Wito huo umetolewa na Mshauri wa Mawasiliano kutoka Kampuni ya Kengo, Niwaeli Gittens-Mbaga, wakati akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kuendeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia kwenye siku ya pili ya warsha ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari pamoja na maafisa mawasiliano kutoka mikoa, wizara na taasisi mbalimbali za Serikali inayofanyika mkoani Morogoro.

Katika mada yake,  Gittens-Mbaga alieleza kuwa mafanikio ya kampeni za nishati safi ya kupikia yanategemea kwa kiwango kikubwa uwezo wa wadau wa mawasiliano kuanzisha na kudumisha mahusiano yenye tija na taasisi, washirika wa maendeleo pamoja na sekta binafsi zinazoweza kuchangia rasilimali na utaalamu.

Aidha, aliwapa washiriki mbinu za kuandaa mapendekezo ya miradi (project proposals) yanayokidhi mahitaji ya wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuzingatia vipaumbele na maslahi ya kila mdau ili kuongeza nafasi ya kupata ushirikiano na ufadhili wa utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Baada ya sehemu ya nadharia, washiriki walishiriki mazoezi ya vitendo kwa kugawanywa katika makundi tofauti, ambapo kila kundi liliandaa pendekezo la mradi wa mawasiliano kuhusu nishati safi ya kupikia na kuliwasilisha mbele ya wawezeshaji pamoja na washiriki wengine.

Uwasilishaji huo uliambatana na mjadala na mrejesho wa kitaalamu uliolenga kuboresha ubora wa mapendekezo hayo, huku washiriki wakipata fursa ya kuimarisha uelewa wao kuhusu mbinu bora za kushirikisha wadau na kutumia mawasiliano yenye matokeo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Warsha hiyo inaendelea kuwajengea washiriki uwezo wa kitaalamu ili kuwawezesha kuandaa na kusambaza maudhui sahihi yatakayochochea uelewa wa jamii na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufikia malengo ya ajenda hiyo nchini.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...