Na George Maziku, Nyang'hwale


MGODI wa wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Mwamakiliga, unaopatikana Kijiji cha Mwamakiliga, kata ya Izunya, wilaya ya Nyang'hwale, Mkoani Geita umewawezesha zaidi ya watanzania 6000 kujiajiri kwenye kazi mbalimbali mgodini hapo na kujipatia kipato.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mgodini hapo, Meneja msaidizi wa mgodi huo Mashaka Kulwa Chitela amesema wananchi kutoka ndani na nje ya wilaya ya Nyang'hwale na mkoa wa Geita wamenufaika kwa kujipatia kazi mbalimbali.

Amesema kuwa wananchi hao wanajishughulisha na kazi za uchimbaji, uokotaji wa mawe ya dhahabu(maarufu ukwale), biashara ya mitambo ya kusaga mawe (crushers), ubebaji wa mifuko ya mawe, boda boda, mama lishe, biashara ya nyumba za kupangisha, maduka, na nyingine nyingi.

"Mgodi wetu umeisaidia sana serikali katika kupunguza idadi ya watanzania wasio na ajira, hapa kuna umati wa zaidi ya watu 6000 wanaojipatia riziki zao za Kila siku. Wapo wachimbaji, kina mama wa ukwale, makago wanaobeba na kupakia mifuko ya mawe, boda boda, mama lishe, wenye gesti, maduka na wafanyabiashara wengine wengi", amesema Chitela.

Ameongeza kuwa, "Tumetengeneza ajira za uhakika zaidi ya 100 katika kada za ukaguzi, ulinzi, ulipuaji na uhudumu wa ofisi. Tuna imani kubwa kwamba tukipata leseni ya uchimbaji tutazalisha ajira Nyingi zaidi."

Amebainisha miongoni mwa watu walionufaika na mgodi huo ni wakazi wa kijiji cha Mwamakiliga na kata ya Izunya ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele katikà nafasi mbalimbali za kazi zinazojitokeza mgodini hapo.

" Tumekuwa na upendeleo maalum kwa wananchi wa kijiji hiki ambao ni wenyeji wetu, walinzi wengi wa mgodi wetu wanatoka hapa Mwamakiliga. Pia tumechukua vijana 25 wa hapa kijijini na Kisha kuwafundisha kazi ya ukaguzi wa migodi", amesitiza Chitela.

Amefafanua mbali na kuzalisha ajira hizo, mgodi wake umekuwa chanzo cha uhakika cha mapato ya halmashauri ya wilaya ya Nyang'hwale kupitia ushuru mbalimbali ikiwemo ushuru wa huduma.

Amesema hata Serikali kuu imekuwa ikinufaika na uwepo wa mgodi huo kupitia malipo ya mrabaha, ambayo ni asilimia 3 kwa kila mifuko 100 ya mawe yenye dhahabu.

"Serikali imetuamini na kutukabidhi jukumu la kusimamia na kukusanya mapato yake katika mgodi huu, kazi hiyo tumekuwa tukiifanya kwa uaminifu mkubwa. Halmashauri yetu ya Nyang'hwale na serikali kuu wote wanapata mapato yao bila ubabaishaji", amebainisha Chitela.

Kuhusu usalama wa mgodi wake kwa wachimbaji na watu wengine wanaofanya kazi mgodini hapo, Chitela amesema suala la usalama kwao ni kipaumbele namba moja, na kwamba mgodi huo haujawahi kupata ajali yoyote kubwa kutokana na umakini wao mkubwa katika usalama.

"Mgodi wetu ni salama kabisa, kwetu suala la usalama ni kipaumbele cha kwanza na idara yetu ya ukaguzi ina watu wa kutosha na makini. Ukaguzi wa duara unafanyika wakati wote mchana na usiku, masaa 24 na mara ikibainila kama duara fulani ni hatarishi, tunasimamisha moja uchimbaji mpaka marekebisho yafanyike",amesema.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...