-Teknolojia, usuluhishi wa migogoro na maboresho ya sheria vipaumbele vya mafunzo
-Mawakili wakumbushwa kulinda maslahi ya Taifa, uwekezaji na usalama wa nchi
-Mafunzo yatekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kupitia na kuboresha sheria
Na Vero Ignatus, Michuzi TV – Arusha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, leo Julai 14, 2026 amefungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa mawakili 650 wa Serikali yanayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC). Mafunzo hayo yanalenga kuwaimarisha mawakili katika utekelezaji wa majukumu yao sambamba na maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Johari alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili kuhusu mabadiliko yanayotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, pamoja na kuhakikisha mfumo wa sheria unaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ili uwe kichocheo cha maendeleo ya Taifa.
Alisema mada zitakazojadiliwa zinahusisha usuluhishi wa migogoro, hususan migogoro ya kibiashara, namna ya kuweka uwiano kati ya maendeleo ya nchi na ulinzi wa wawekezaji, pamoja na kutathmini kama sheria zilizopo zinachochea mageuzi ya uchumi na maendeleo endelevu.
"Tunataka pia kuangalia jukumu la wakili katika kuimarisha uzalendo, kulinda maslahi pamoja na usalama wa Taifa. Wasipofahamu wajibu huo wanaweza kujikuta wanaingia katika matendo yanayoweza kuhatarisha usalama wa Taifa au kuathiri maslahi ya nchi kiuchumi na kijamii," alisema Mhe. Johari.
Awali, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Sheria, Wakili Neema Ringo, alisema mafunzo hayo yatawawezesha mawakili kuongeza uelewa kuhusu matumizi ya teknolojia, kutambua vihatarishi vinavyotokana na maendeleo ya kidijitali, pamoja na kujadili namna ya kuboresha sheria ili ziendane na mazingira ya sasa.
Alieleza kuwa mafunzo hayo pia yanatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyemtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuratibu mapitio ya sheria zote ili kufanyiwa marekebisho, kuboreshwa au kufutwa pale zinaposhindwa kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Wakili Ringo aliongeza kuwa mafunzo hayo, yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yanatoa fursa kwa mawakili kubadilishana uzoefu, kuongeza ujuzi na kujadili mabadiliko ya sheria, sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorious Njole, alisema jumla ya mawakili 650 kutoka wizara, taasisi za Serikali, mamlaka za Serikali za Mitaa na idara mbalimbali za umma wanashiriki mafunzo hayo. Alisema lengo ni kuwajengea uwezo wa kitaaluma na kiutendaji ili waendelee kusimamia kwa ufanisi tasnia ya sheria na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...