Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika shule zenye mkondo wa elimu ya amali, likieleza kuwa ndiyo njia sahihi ya kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi itakayochochea maendeleo ya uchumi wa Taifa

Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Dar es Salaam.

Dkt. Lingwanda alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa NACTVET kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu majukumu ya Baraza, huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja na kupokea maoni na ushauri wa kuboresha utendaji wake.

"Maonesho haya yanatupa nafasi ya kuwafikia wananchi moja kwa moja, kuwaelimisha kuhusu elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na huduma zinazotolewa na Baraza. Pia tunapata fursa ya kusikiliza maoni yao ili kuendelea kuboresha huduma zetu," alisema.

Alisema NACTVET imeridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi wanaotembelea banda lake, ambapo wengi wamepata taarifa na huduma walizokuwa wakizihitaji kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.

Dkt. Lingwanda alibainisha kuwa moja ya vivutio vikubwa katika banda la NACTVET mwaka huu ni ushiriki wa wanafunzi wa shule za amali wanaoonesha kwa vitendo ujuzi walioupata kupitia kazi mbalimbali za ubunifu na uzalishaji.

Alieleza kuwa uwezo unaooneshwa na wanafunzi hao unathibitisha kuwa elimu ya amali huwajengea wahitimu uwezo wa kuingia moja kwa moja katika soko la ajira au kujiajiri mara wanapomaliza masomo yao.

"Hawa vijana wanaonesha kwa vitendo matokeo ya elimu wanayoipata. Hii ni ishara kwamba elimu ya amali inawajengea uwezo wa kufanya kazi, kuzalisha na kujitegemea mara baada ya kuhitimu," alisema.

Alisisitiza kuwa mafunzo ya ufundi na elimu ya amali yana mchango mkubwa katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kujiajiri, kuajiriwa, kubuni teknolojia mpya na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

Aidha, aliwataka wawekezaji na wadau wa sekta ya elimu kutumia fursa zilizopo kuanzisha shule na taasisi zinazotoa elimu ya amali na mafunzo ya ufundi stadi, akibainisha kuwa NACTVET ipo tayari kutoa ushauri na kuwaelekeza kuhusu taratibu zote zinazohitajika.

Akizungumzia mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa, Dkt. Lingwanda alisema elimu ya ufundi na mafunzo ya amali ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kuongeza uzalishaji, biashara na maendeleo ya viwanda.

Aliongeza kuwa wingi wa bidhaa zinazozalishwa na Watanzania na kuoneshwa katika Maonesho ya Sabasaba ni ishara kuwa nchi inaendelea kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji na ujuzi wa wananchi wake, hali inayochochea ajira, ukuaji.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...