
*Yawahimiza wananchi kutembelea banda
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limewahimiza wananchi kutembelea banda lake katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) ili kujionea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa elimu ya amali na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Banda hilo limekuwa kivutio kutokana na uwepo wa wanafunzi kutoka shule za sekondari zenye mkondo wa amali, ambao wanaonesha kwa vitendo ujuzi, ubunifu na maarifa waliopata kupitia masomo yao.
Wanafunzi hao wanawasilisha kazi mbalimbali zinazoonyesha namna elimu hiyo inavyowaandaa kujiajiri, kuajirika na kuendelea na masomo ya juu wakiwa na msingi imara wa taaluma.
Mbali na maonesho ya vitendo, wataalamu wa NACTVET wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya Baraza katika kusimamia ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na kueleza fursa za masomo zinazopatikana katika vyuo vinavyosimamiwa na Baraza.
Pia wananchi wanapatiwa maelezo kuhusu taratibu za udahili, matumizi ya Namba ya Utambuzi na Tuzo (AVN), upatikanaji wa hati za matokeo na huduma nyingine zinazotolewa na Baraza kwa lengo la kuboresha utoaji wa elimu nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari Baobab, Careen Maki, alisema mkondo wa amali umemjengea uwezo na kujiamini katika kufikia ndoto yake ya kuwa mhandisi wa umeme.
Alisema kwa sasa anasomea fani ya umeme kupitia mkondo wa amali, jambo ambalo linampa msingi mzuri wa kuendelea na elimu ya juu na kutimiza malengo yake ya kitaaluma.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bwiru mkoani Mwanza, Daud Elias, alisema anasomea fani ya ujenzi kupitia mkondo wa amali na anaamini elimu hiyo itamwezesha kutimiza ndoto yake ya kuwa Mhandisi wa Majengo.
Alieleza kuwa utofauti wa mkondo wa amali ni kwamba unampa mwanafunzi nafasi ya kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia, hali inayoongeza uelewa, kujiamini na uwezo wa kutatua changamoto zinazohusiana na taaluma husika.
NACTVET imesema maonesho ya Sabasaba ni jukwaa muhimu kwa wazazi, wanafunzi, walimu, waajiri na wadau mbalimbali kujifunza kuhusu mchango wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi katika kuzalisha wataalamu wenye ujuzi, kukuza ubunifu, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.NACTVET yaonesha mafanikio ya elimu ya amali Sabasaba


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...