Dar es Salaam, 1 Julai 2026 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inapenda kuufahamisha Umma wa Watanzania kuwa tarehe 30 Juni 2026, imekabidhi Serikalini mchango wa TZS 61,053,535,363 ikiwa ni fedha za makusanyo yake katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Jamuhuriy a Muungano wa Tanzania ya kuleta maendeleo kwa wananchi. 

Mchango huo ulikabidhiwa kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika hafla ya upokeaji wa gawio na michango ya Taasisi za Umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. 

Katika hafla hiyo, NIDA pia ilipata heshima ya kutunukiwa tuzo baada ya kushika nafasi ya pili miongoni mwa Taasisi zilizofanya vizuri katika kuwasilisha mchango wake Serikalini. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Mheshimiwa Rais, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa NIDA katika kuimarisha mapato ya Serikali na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi. 

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji amesema mafanikio hayo ni matokeo ya kuendelea kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi. 

“Tunapokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Mchango huu siyo tu takwimu za kifedha, bali ni matokeo ya uboreshaji wa huduma za utambuzi wa Taifa ambapo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha usalama, kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kichocheo cha mapato katika sekta binafsi na Umma,” amesema Kaji. 

NIDA inaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusajili na kuwatambua wananchi kwa kutoa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) na Vitambulisho vya Taifa, pamoja na kuwezesha matumizi ya taarifa sahihi za utambuzi katika sekta mbalimbali za huduma za umma na binafsi.

 Utambuzi wa Taifa ni msingi muhimu katika kuwezesha Serikali na Sekta Binafsi kupanga, kuhudumia wananchi au wateja wake kwa ufanisi, kuimarisha usalama, kudhibiti mianya ya udanganyifu na kuongeza tija katika utoaji wa huduma. NIDA inatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono, miongozo na uwekezaji unaoendelea kufanywa katika kuimarisha mifumo ya utambuzi nchini.

  Aidha, NIDA inawashukuru wananchi, wadau, taasisi za Serikali na sekta binafsi kwa kuendelea kushirikiana na Mamlaka katika kujenga Taifa lenye utambuzi sahihi, huduma bora na maendeleo jumuishi. Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano na Hifadhi Hati 




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...