Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema maridhiano ya kisiasa hayapaswi kutafsiriwa kama udhaifu, bali ni ishara ya ukomavu wa kisiasa unaoweka msingi imara wa umoja, amani na kuheshimiana katika jamii.
Akihutubia katika hafla ya utiaji saini wa Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar iliyofanyika visiwani Zanzibar leo, Alhamisi Julai 9, 2026, Rais Samia alisema viongozi wanaweza kuwa na mitazamo tofauti, lakini wakaunganishwa na dhamira ya kulinda maslahi ya taifa na ustawi wa wananchi.
Ameeleza kuwa maridhiano yanaonyesha uwezo wa viongozi kujadili hoja zinazowatofautisha kwa hekima, huku wakikubaliana katika masuala ya msingi yanayohusu uongozi na maendeleo ya nchi.
Rais Samia alisema hatua hiyo inafungua ukurasa mpya wa kuimarisha umoja, mshikamano, utulivu na amani kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa jitihada hizo zinapaswa kuendelezwa na kuenziwa.
“Hakika jitihada hizi zinahitaji kuendelezwa na kuenziwa. Nimesema jambo hili la kiungwana kwa kuwa uungwana unatufunza siasa za kushindana kwa hekima na si kwa kupaza sauti bila mantiki,” amesema Rais Samia.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi na wadau wa siasa kuendelea kujenga utamaduni wa mazungumzo, kuheshimiana na kuweka mbele maslahi ya taifa ili kudumisha amani na kuharakisha maendeleo ya wananchi.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...