Kampuni ya SUHARA Logistics Company Limited imesema ushiriki wake katika Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026) umeiwezesha kukutana na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, kupanua mtandao wa kibiashara na kuongeza fursa za ukuaji wa kampuni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Julai 23, 2026, Meneja wa Miradi kutoka SUHARA Logistics Company Limited, Amina Abdallah, amesema kampuni hiyo inatoa huduma za usafirishaji wa mizigo kutoka eneo la chanzo hadi sehemu anayoelekeza mteja kwa kuzingatia viwango vya usalama na ubora.

Amesema kwa sasa kampuni inashirikiana na Mgodi wa GGML katika kusafirisha mizigo mbalimbali na imefanikiwa kuhakikisha mizigo yote inawafikia wateja salama, aidha kampuni ina ofisi katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza pamoja na maghala (warehouses) kwa ajili ya kuhifadhi mizigo inayosubiri kukamilisha taratibu za malipo.

Amina amesema tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo haijawahi kuripotiwa ajali wala changamoto kubwa katika shughuli zake za usafirishaji, jambo linalodhihirisha dhamira ya kampuni katika kutoa huduma salama na zenye kuaminika.

Aidha, amesema ukuaji wa sekta ya madini nchini unaendelea kuvutia wawekezaji wengi, hali inayochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa, kutokana na hilo, SUHARA imeona umuhimu wa kushiriki jukwaa hilo ili kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali na kujitangaza zaidi katika sekta ya madini.

Kwa upande wake, Mwangalizi wa Tawi la SUHARA Mkoa wa Mwanza, Sarah Utiku, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuandaa Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026), akisema limekuwa fursa muhimu kwa kampuni kuonyesha huduma zake kwa wadau wa sekta hiyo.

Sarah amesema kampuni imechangia maendeleo ya jamii kwa kutoa ajira ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi wake ni Watanzania. Pia imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii ikiwemo kutoa misaada katika shule, kutembelea vituo vya watoto yatima na kushiriki shughuli nyingine za kijamii.

Ameongeza kuwa SUHARA imejijengea sifa kutokana na ubora wa huduma zake za usafirishaji wa mizigo kutoka kwa muuzaji hadi kwa mnunuzi pamoja na kusimamia taratibu zote za forodha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ufanisi, hivyo kuhakikisha mizigo inawafikia wateja kwa wakati na kwa usalama.

Aidha, amewakaribisha wadau wa sekta ya madini kutembelea banda la SUHARA katika jukwaa hilo ili kujifunza kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni, huku akibainisha kuwa jukwaa hilo pia limeipa kampuni nafasi ya kujifunza kutoka kwa wadau wengine na kuboresha huduma zake.

Pia amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kufanya kazi kwa bidii, akieleza kuwa sera nzuri zilizowekwa na Serikali zimeendelea kuvutia wawekezaji na kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania.

Naye Mkurugenzi wa SUHARA Logistics Company Limited, Anand Barchha, amesema huduma za uhifadhi wa mizigo (warehousing) ni sehemu muhimu ya mnyororo wa ugavi katika ununuzi na usambazaji wa bidhaa, na  kampuni imeweka mifumo na viwango bora vya usimamizi wa maghala na bidhaa ili kuhakikisha usimamizi mzuri wa shehena, utoaji wa mizigo kwa wakati ndani na nje ya nchi, pamoja na kuongeza ufanisi wa mnyororo wa ugavi na kuwapa wateja utulivu na imani katika huduma wanazopata.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...