TANZANIA inalenga kuongeza ushiriki wake katika soko la kimataifa la kaboni, huku kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kikipewa jukumu la kuimarisha usimamizi, kuvutia uwekezaji wa kijani na kuongeza manufaa ya rasilimali za asili.
Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema Tanzania inapaswa kubadilika kutoka kuwa mshiriki wa kawaida katika biashara ya kaboni na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kujenga mifumo thabiti itakayowezesha utekelezaji wa miradi ya kaboni yenye uadilifu wa hali ya juu.
Katibu Huyo Mkuu amesema hayo Julai 21 2016 jijini Dar es Salaam kwenye kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo Cha Kaboni nchini kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Dkt. Muyungi amesema ukuaji wa uchumi wa kaboni duniani ni fursa muhimu kwa Tanzania kuongeza mapato ya Taifa sambamba na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Changamoto yetu sasa siyo kushiriki tu katika masoko ya kaboni, bali kuyaongoza,” alisema Dkt. Muyungi.
Amesema soko la kaboni duniani linaendelea kukua kwa kasi na sasa linakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 107 kwa mwaka, huku Afrika ikiwa na uwezo wa kuzalisha takribani dola bilioni 6 kwa mwaka ifikapo 2030 endapo itatumia kikamilifu fursa zilizopo.
Dkt. Muyungi amesema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kutokana na utajiri wa rasilimali zake ikiwemo misitu, maeneo oevu, mifumo ya ikolojia ya pwani na bahari, pamoja na fursa zilizopo katika nishati safi na kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kuwa hadi sasa Tanzania imesajili miradi 99 ya kaboni, huku zaidi ya mikopo ya kaboni milioni 13.4 ikiwa imetolewa. Hata hivyo, amesema mafanikio hayo bado hayajaakisi thamani halisi ya kiuchumi inayoweza kupatikana kupitia sekta hiyo.
“Mafanikio haya hayaoneshi manufaa yote tunayotarajia kutoka kwenye sekta ya kaboni. Tunahitaji kufanya zaidi kuhakikisha miradi inafikia hatua ya utekelezaji na kuanza kuleta thamani kwa Taifa na jamii zetu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Muyungi aliitaka bodi ya Kituo hicho kuimarisha mifumo ya usajili wa miradi ya kaboni, kuharakisha utekelezaji wa mifumo ya Ibara ya 6 ya Mkataba wa Paris kuhusu biashara ya kaboni na kuboresha mifumo ya Upimaji, Utoaji wa Taarifa na Uhakiki (MRV) ili kuongeza uwazi na kuimarisha imani ya wawekezaji.
Aidha, alisema Kituo hicho kinapaswa kuhakikisha manufaa yatokanayo na miradi ya kaboni yanagawanywa kwa haki, hasa kwa jamii zinazoshiriki katika uhifadhi wa mazingira, huku kikijenga uwezo wa wataalamu wa ndani katika mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya kaboni.
“Tanzania lazima ijenge mfumo wa soko la kaboni unaovutia uwekezaji, unaolinda uadilifu wa mazingira na kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa zinazotokana na sekta hii,” alisema.
Alisema usimamizi madhubuti wa sekta ya kaboni utachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji wa kijani, kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuchochea maendeleo endelevu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Muyungi aliitaka Menejimenti ya Kituo Cha Kaboni kukamilisha kwa haraka mifumo muhimu ya uendeshaji, ikiwemo kuboresha Mfumo wa Usajili wa Kaboni (Carbon Registry), kuwasilisha Mpango Mkakati wa Kituo na kuimarisha mifumo ya kitaasisi.
Pia aliitaka bodi ya Kituo hicho kuandaa taarifa ya kina kuhusu miradi yote ya kaboni iliyosajiliwa na ile iliyoanza utekelezaji kati ya Januari na Julai 2026, ikionesha hatua iliyofikiwa, kiwango cha uwekezaji na manufaa yanayotarajiwa kwa Taifa na wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Kaboni, Dkt. Albina Chuwa, ameahidi kutekeleza maelekezo hayo na kuongeza uelewa wa umma kuhusu biashara ya kaboni nchini, sambamba na kuimarisha utawala bora katika sekta hiyo.
Kituo cha Kaboni kilianzishwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira kwa lengo la kuratibu ufuatiliaji wa kaboni, kuimarisha usimamizi wa masoko ya kaboni na kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika fursa za fedha za tabianchi duniani.



.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...