Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, imeamuru Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage, aachiwe kwa dhamana kuanzia Julai 21, 2026, wakati uchunguzi wa tuhuma za uchochezi zinazomkabili ukiendelea.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Joachim Tiganga wakati wa usikilizwaji wa Shauri Na. 15653/2026.

Kaijage amekuwa akishikiliwa katika Kituo cha Polisi Chang’ombe akituhumiwa kuhamasisha maandamano yaliyojulikana kama “Sabasaba.”

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, upande wa Serikali uliieleza Mahakama kuwa haukuwa na pingamizi dhidi ya ombi la dhamana, na kwamba taratibu za kumwachia mshtakiwa zinaweza kuendelea kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa Kaijage, Prosper Malangalila, alidai kuwa mteja wake alikaa mahabusu kwa siku 12 bila kufikishwa mahakamani, licha ya kosa analotuhumiwa kuwa la dhamana. Aliiomba Mahakama iamuru mteja wake aachiwe kwa dhamana, alipwe fidia kwa kuzuiliwa kwa muda huo, na Serikali ilipe gharama za maombi hayo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama ilikubali ombi la dhamana na kuamuru Kaijage aachiwe kwa masharti ya dhamana. Hata hivyo, ilikataa ombi la kulipwa fidia kwa kipindi alichokuwa mahabusu.

Mahakama imeeleza kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, Kaijage atafikishwa mahakamani kujibu rasmi tuhuma zinazomkabili.

Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili Prosper Malangalila amesema upande wake umepokea uamuzi huo na utaendelea kufuatilia hatua zinazofuata za kisheria katika shauri hilo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...