.jpeg)
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akikata utepe (kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma za Next Generation Sequencing (NGS) unaoashiria enzi mpya ya tiba ya jenomiki, ukikiweka Chuo Kikuu kuwa kitovu cha kitaifa na kikanda cha sayansi ya jenomiki, uchunguzi wa kisasa wa magonjwa, utafiti na ubunifu. anayeshuhudia katikati ni Makamu Mkuu wa chuo cha MUHAS, Profesa, Appolinary Kamuhabwa.
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
SERIKALI imewataka wanasayansi na wataalamu wa afya kuziba pengo lililopo kati ya tiba asili na tiba ya kisasa kwa kufanya tafiti za kisayansi zitakazothibitisha usalama na ufanisi wa tiba za asili ili ziweze kuingizwa rasmi katika mfumo wa huduma za afya nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Kisayansi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) uliofanyika leo Julai Mosi, 2026 katika kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.
Prof. Mkenda amesema ni muhimu kubadili matumizi ya tiba za asili zinazotumiwa na wananchi kuwa tiba zinazotegemea ushahidi wa kisayansi kupitia tafiti, majaribio ya kitabibu na uthibitisho wa kitaalamu.
Amesema madai yote kuhusu ufanisi wa tiba, yakiwemo yale ya tiba za asili, yanapaswa kuthibitishwa kisayansi ili kubaini usalama wake, kiwango sahihi cha matumizi na aina ya wagonjwa wanaoweza kunufaika nazo.
“Lengo si kupinga tiba asili, bali kuziinua kupitia sayansi ili zitumike kwa usalama ndani ya mfumo wa huduma za afya,” amesema.
Aidhqla, Prof. Mkenda ameibainisha kuwa Serikali itaratibu warsha za kitaifa zitakazowakutanisha watafiti, waganga wa tiba asili, wadhibiti na wataalamu wa haki miliki ili kuweka mfumo wa kutathmini na kulinda maarifa ya tiba za asili.
Pia, ameonya kuwa kutegemea ushuhuda usiofanyiwa uthibitisho wa kisayansi kunaweza kuwaweka wagonjwa katika hatari ya kutumia tiba zisizo salama au zisizo na ufanisi, akisisitiza umuhimu wa majaribio ya kitabibu, uchunguzi wa maabara na tafiti za kina kabla ya tiba yoyote kukubalika.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la MUHAS, Makata Yambi, amesema ubunifu na tafiti zinazozalishwa nchini zina nafasi muhimu katika kuimarisha mfumo wa afya, huku mkutano huo ukiwa jukwaa la watafiti, watunga sera na wadau wa maendeleo kubadilishana uzoefu na kutafuta suluhisho la kuboresha huduma za afya kwa wote.
Naye, Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo kinawekeza katika teknolojia za kisasa ikiwemo akili bandia (AI), genomiki na uchunguzi wa magonjwa kwa mbinu za kisasa ili kuimarisha tafiti na utoaji wa huduma za afya.
Amesema kuanzishwa kwa huduma za uchunguzi wa kizazi kipya wa vinasaba (Next Generation Sequencing) kunaifanya MUHAS kuwa kitovu cha kikanda katika sayansi ya jenomu na tiba mahsusi, hatua itakayosaidia pia kutathmini kwa kina tiba zinazotokana na maarifa ya tiba asili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Kisayansi wa MUHAS, Prof. Raphael Sengeja, amesema mwaka huu mkutano umepokea jumla ya tafiti 247, zikiwemo 138 za uwasilishaji wa moja kwa moja na 109 za mabango, zikihusu tiba asili, akili bandia, genomiki, afya ya uzazi, usugu wa vimelea dhidi ya dawa na uimarishaji wa mifumo ya afya.
Amesisitiza kuwa lengo la mkutano huo ni kuhakikisha tafiti zinazofanywa hazibaki kwenye machapisho ya kitaaluma pekee, bali zinatafsiriwa kuwa suluhisho halisi litakaloboresha afya na ustawi wa jamii.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...