*Aipongeza TASAC kutoa gawio la Zaidi ya sh.bilioni 20

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeihakikishia sekta ya usafiri wa majini kuwa itaendelea kulinda uwekezaji wa vyombo vya majini na mali za wawekezaji ili kuimarisha mazingira salama ya biashara, huku ikiitaka Tanzania Shipping Agencies Corporation (TASAC) kuongeza juhudi katika kuzalisha wataalamu wa sekta ya bahari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, baada ya kutembelea banda la TASAC katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Kihenzile amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wawekezaji wanaowekeza katika meli, boti na vyombo vingine vya majini wanaendelea kufanya shughuli zao kwa usalama, huku ulinzi wa wananchi, wageni na mali zao ukipewa kipaumbele kupitia taasisi husika.

Amesema mazingira hayo salama yataendelea kuongeza imani ya wawekezaji na kuvutia uwekezaji zaidi katika uchumi wa buluu, ambao ni moja ya sekta muhimu zinazochochea ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Katika hatua nyingine, Kihenzile ameipongeza TASAC kwa mafanikio yake ya kifedha baada ya kutoa gawio la Shilingi bilioni 20.45, sawa na asilimia 15 ya mapato ghafi ya shirika kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambalo lilikabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema kiwango hicho cha gawio kinaonyesha shirika linafanya kazi kwa ufanisi na kuwataka viongozi na watumishi wake kuendelea kusimamia majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji ili kuongeza mchango wa taasisi hiyo katika uchumi wa Taifa.

Akizungumzia ukuaji wa sekta ya usafiri wa majini, Kihenzile amesema ongezeko kubwa la biashara katika bandari za Tanzania limeongeza mahitaji ya wataalamu wa sekta ya bahari, akibainisha kuwa kiwango cha mizigo kilichokuwa kinatarajiwa kufikiwa mwaka 2030 kilifikiwa mapema mwaka 2022 kutokana na uongozi madhubuti, kuimarika kwa diplomasia ya uchumi na ushiriki wa sekta binafsi.

Amesema ukuaji huo unamaanisha kuwa kutahitajika idadi kubwa zaidi ya manahodha, mabaharia, wasaidizi wa mabaharia pamoja na wataalamu wengine wa usafiri wa majini ili kuhudumia shughuli zinazozidi kupanuka.

Kutokana na hali hiyo, ameihimiza TASAC kutotekeleza jukumu la udhibiti pekee, bali kushirikiana na Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaoweza kukidhi mahitaji ya sekta ya bahari inayokua kwa kasi.

Aidha, amewapongeza watumishi wa TASAC kwa uadilifu na weledi wanaouonyesha katika utekelezaji wa majukumu yao, akiwataka kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo ili kuhakikisha sekta ya bahari inatoa manufaa makubwa kwa Watanzania na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...