NA DENIS MLOWE IRINGA


TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Kifulilo kimesema ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika mkoani Iringa kwa mara ya kwanza unalenga kuwafikishia wakulima teknolojia mbalimbali za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kipato.

Hayo yameelezwa na Mratibu wa Kitengo cha Uhamishaji wa Teknolojia na Ushirikiano wa TARI Kifulilo, Lilian Ngusi kuwa taasisi hiyo ina vituo vya utafiti 20 nchini, huku Mkoa wa Iringa ukiwa na Kituo cha TARI Kifulilo pamoja na vituo vidogo vya Satondale kilichopo Ipogolo na Isimani.

Alisema kupitia maonesho hayo, TARI imeleta teknolojia mbalimbali za kilimo, ikiwemo mbegu bora, miche ya matunda, mazao ya mfano na bidhaa zilizoongezwa thamani ili kuwahamasisha wakulima kutumia matokeo ya tafiti katika shughuli zao za uzalishaji.

Ngusi amesema taasisi hiyo inafanya tafiti kwenye mazao mbalimbali ikiwemo viazi mviringo, viazi lishe, maharage, soya na parachichi, huku ikitoa ushauri kwa wakulima kuhusu mbinu bora za uzalishaji na namna ya kuongeza thaưmani ya mazao yao.

Ameeleza kuwa kwa zao la viazi mviringo, wakulima wanashauriwa kutengeneza bidhaa kama chipsi badala ya kuuza mazao ghafi pekee, hatua inayoweza kuongeza mapato yao.

Kwa upande wa viazi lishe, amesema TARI imefanikiwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo mikate na tambi, ambazo zinaongeza matumizi ya zao hilo pamoja na thamani yake sokoni.

Aidha, amesema taasisi hiyo ina aina mbalimbali za mbegu bora za maharage na soya, huku mbegu ya soya aina ya Uyole ikitumika kutengeneza uji wenye lishe kutokana na kiwango kikubwa cha protini kilichopo kwenye zao hilo.

Aliongeza kuwa TARI pia inazalisha miche bora ya parachichi ya aina mbalimbali na kuwapatia wakulima elimu ya namna ya kuikuza, kuitunza, kuongeza uzalishaji na kukabiliana na wadudu waharibifu.

Aidha alisema kuwa taasisi hiyo imeleta pia mitego maalumu ya kunasa wadudu waharibifu wa matunda pamoja na teknolojia nyingine zinazowasaidia wakulima kupunguza hasara na kuongeza tija mashambani.

Amesisitiza kuwa lengo la TARI ni kuhakikisha teknolojia zinazozalishwa kupitia tafiti zinawafikia wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao, usalama wa chakula na kuinua kipato cha wananchi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...